Tuesday, September 25, 2012

HERI YAO

Katika jamii yetu ni kawaida sana kusikia mtu akisema "heri yao" huku akiendelea kwa kutaja baadhi ya mambo au vitu ambavyo pengine ni muhimu sana katika maisha tunayoishi lakini katika ufalme wa mbingu si chochote......kwa mfano,ni kawaida kusikia mtu akisema heri ya wale wenye pesa nyingi,heri ya wale wenye elimu,heri ya wale wenye ajira au heri ya wale wenye afya njema na mambo mengine kadha wa kadha.......katika maisha yake mwokozi wetu yesu kristu aliishi maisha bila dhambi na maisha yake tangu kuzaliwa, kusulubiwa, kufufuka hadi kupaa kwake mbinguni, kristu alionyesha namna mungu alivyo na upendo,huruma hata nguvu na uweza uliotukuka ndiyo sababu aliitwa "Emmanuel" likiwa na maana "Mungu pamoja nasi"

Matendo yake,mwenendo wake, uweza wake  hata maneno yake kristu ni kielelezo juu ya matendo,mwenendo na uwezo wa mungu. Basi ni dhahiri kwamba maneno aliyoyatamka mwokozi wetu yesu kristu hakika ni maneno toka kwa mungu mwenyezi na moja katika ya maneno muhimu aliyoyatamka ni yale ambayo aliyotamka wakati akiwafundisha wanafunzi wake pale kilimani akisema.

HERI YAO MASIKINI WA ROHO
Katika mstari huu,kristu alimaanisha wale wenye kutambua umasikini wao katika mambo ya kiroho,mambo yahusuyo mwenyezi mungu na ufalme wa mbingu kwa ujumla,watu hawa wapo tayari kusikiliza,kusoma,kutafakari,kuamini na kulitenda neno la mungu.Watu hawa waliotambua umasikini wao wa kiroho ndiyo ambao mungu huwapa uwezo wa kutambua mambo hayo kwani "mwanadamu wa kawaida hatambui mambo ya kiroho,ni kama upuuzi kwake na kamwe hawezi kuyaelewa kwani hutambuliwa kiroho.

HERI YAO WENYE HUZUNI
Huzuni yaweza kusababishwa na matatizo,magonjwa,mateso pia majaribu ya hii dunia,katika neno lake mungu baba ameweka wazi kuwa chanzo cha yote hayo ni dhambi, hivyo huzuni husababishwa na dhambi ndiyo maana kristu alisema heri wenye huzuni lakini hii ni kwa wale waliotambua chanzo cha huzuni hiyo kuwa ni dhambi na kuamua kutubu na kupokea wokovu kwa kumwamini na kumfuata yesu.

HERI YAO WAKARIMU
kweli, wacheshi na wapole twaweza kuwaweka katika kundi la wakarimu,lakini katika mafunzo yake pale kilimani kwa wanafunzi wake yesu kristu alisema hata ukawa na imani ya kuweza kuhamisha milima, kama huna upendo ni sawa na bure,ukarimu huu alioumaanisha bwana ni hali ya kuwa na upendo kwa wanadamu wenzetu,alisema mpende jirani yako kama unavyojipenda pia akasisitiza mpende adui yako.

HERI YAO WENYE NJAA NA KIU YA UTAKATIFU
Biblia inasema "hakuna mwanadamu awezae kuishi maisha bila dhambi bali mmoja tu aliye mtakatifu"naye ni bwana wetu yesu kristu,lakini bwana alisema kuwa, heri ya wale ambao mioyo yao ina njaa na kiu kubwa ya kuishi maisha takatifu,maisha ya kumpendeza mungu,maisha katika kristu,biblia inaendelea kusema kuwa "watakatifu watapimwa kwa imani"hivyo twaweza potoka katika dhambi lakini imani yetu i ndani ya kristu na kwamba amezilipa dhambi zetu zote pale msalabani hivyo kwa kuteswa kwake si tumekuwa watakatifu.

HERI YAO WENYE HURUMA
Tunapoishi maisha katika dunia hii,shida na mateso ni vitu visivyoepukika,maandiko yanasema "katika dunia hii mtapata mateso,lakini vumilieni kwani nimeushinda ulimwengu" ni neno la mungu kuhusu uwepo wa mateso katika maisha yetu,hivyo kristu anasema wale ambao huguswa na mateso ya wengine kama vile wajane,yatima,wagonjwa,waliofungwa,masikini na wote wanaoteseka na shida za hii dunia kwa kuwatembelea,kuwafariji na kuwapatia misaada baraka zao zipo.

HERI YAO WENYE MOYO SAFI
Twaweza kuwa wapole,wacheshi,wakarimu hata wenye upendo lakini tusiwe na mioyo safi....moyo safi hutokana na kupokea zawadi ya wokovu kutoka kwa mungu,zawadi hii ni kumpokea na kumwamini yesu kristu kama mwokozi na mfalme katika maisha yetu,mara baada ya kamwamini yesu kristu mioyo yetu humpokea roho mtakatifu ambaye hutufundisha na kutuwezesha kutenda mema na kuepuka dhambi na hapo ndiyo mioyo yetu inaweza kumpendeza mungu.

HERI YAO WENYE AMANI
Amani moja kati ya matunda ya roho mtakatifu,akiwa ndani yetu hutuwezesha kuwa na imani ndani ya mioyo yetu pamoja na shida,njaa,chuki,wivu,tamaa,vita,magonjwa na tabu tunazokabiliana nazo katika  hii dunia..kristu alipowaambia wanafunzi wake "heri wenye amani" alikuwa anamaanisha amani ya kiroho na si kutokuwepo kwa shida au matatizo ya hii dunia na amani hii ni zao la roho mtakatifu pekee,hivyo kwa wale tuliompokea kristu amani i tele ndani ya mioyo yetu.

HERI YA WALE WANAOHUKUMIWA KWA AJILI YA UTAKATIFU
Tunapoishi maisha katika kristu ni lazima tupambane na upinzani mkubwa kwani biblia inasema "dunia hupenda ya dunia,hivyo mkiona mnachukiwa mjue kuwa nyinyi si wa dunia kwani mngekuwa wa dunia, dunia ingejipenda" ndiyo maana wayahudi hawakuweza kuutambu awakati ambao mwokozi alikuja kupitia jamii yao na wakashindwa kutii maandiko juu ya aliyetabiriwa (kristu) hata wakati mtakatifu Yohana akimbatiza yesu na sauti toka mbinguni ikasikika ikisema "huyu ndiye mwanangu mpendwa,msikilizeni" hawakuamini, matokeo yake wakamhukumu mwana wa mungu na israel ikashindwa kupokea heshima kuwa kitovu cha dunia kwa kushindwa kutambua wakati wa ujio wa kristu.



Katika ufalme wa mbingu kila tendo lina matunda yake liwe jema ua baya,hivyo tunapoishi maisha katika kristu tusichoke kutenda mema kwani baraka na neema za mungu zatufuata popote tuendapo,ni muhimu kukumbuka kuwa twaweza pata matunda mengi mema kwa kutenda mema hapa duniani lakini malipo haswa yatungoja mbinguni pale ambapo mwokozi wetu yesu kristu atakuja tena kutuchukua sisi tulio hai na wale walio wafu watafufuliwa kwenda mbinguni kwa mungu baba.



Japokuwa kristu alipendelea kuwafunza wanafunzi wake kwa mafumbo,lakini hapa aliweka wazi juu ya mambo ambayo mungu atatenda kwa watu wake,hii ni katika kuonyesha umuhimu na msisitizo wa jambo lenyewe, napo akasema.......Heri ya masikini wa roho maana UFALME WA MUNGU NI WAO......Heri yao wenye huzuni maana WATAFARIJIWA........Heri yao wakarimu maana WATARITHI UFALME WA MBINGU.......Heri wenye kiu na njaa ya utakatifu maana WATASHIBISHWA.........Heri wenye huruma maana WATASAMEHEWA........Heri wenye mioyo safi maana WATAMWONA MUNGU.......Heri wenye amani maana WATAITWA WANA WA MUNGU..Heri wanaotengwa na kuhukumiwa kwa ajili ya utakatifu kwa maana UFALME WA MBINGU NI WAO.