Monday, October 1, 2012

UDHAIFU WA SHETANI

Mwenyezi mungu baada ya kumaliza kazi nzito ya kuiumba dunia pamoja na vitu vyote vilivyomo ndani yake,kazi iliyokuwa imebaki ni kutuchukua na kutushirikisha katika maisha ya milele huko mbinguni,kwa kushirikiana na mwanae mpendwa yesu kristu mfalme wa amani ambaye ndiye aliye na mamlaka yote duniani na mbinguni pia,chini yake alikuwa huyu ambaye sisi leo hii tunamtambua kama shetani mfalme wa nguvu za giza.


Upendo wa mungu kwetu sisi wanadamu ni wa ajabu na hauna mfano na mambo aliyotuandalia huko mbinguni hayajawahi ingia akilini wala hayajawahi onekana kwa macho wala masikio yetu hayajawahi kusikia,maandiko yanasema itakuwa furaha na shangwe......Shetani kwa tamaa ya madaraka kwani alitaka kuwa juu ya mwana wa mungu pamoja na wivu kuona kuwa mungu anatupenda sana sisi wanadamu kuliko hata malaika,akaamua kumsaliti muumba na kufanya hivyo aliapa ya kwamba kamwe mimi na wewe tusiuone upendo,baraka,huruma,rehema za mungu pamoja na ufalme wa mbingu.Mungu baba akaamua kumuadhibu kwa kumtupa duniani, kisasi cha mungu kipo juu yake na siku ya mwisho atakwena jehanamu.

HANA MAMLAKA
Maandiko yanasema mbingu na dunia na vyote vilivyo ndani yake vinavyoonekana na visivyoonekana ikiwa ni pamoja na shetani mwenyewe vimeumbwa na mungu na yeye ndiye mwenye mamlaka yote,hakuna kiumbe yeyote aliye juu ya mamlaka aliyoianzisha mungu wa majeshi na kumkabidhi mwanae yesu kristu.

HANA NGUVU
Baada ya kutupwa duniani na mungu,shetani alinyang'anywa nguvu zote na kwamba hana uwezo wa kuukwamisha mpango wa mungu kwetu sisi wanadamu wa kwenda mbinguni,kabla ya ujio wa yesu kristu shetani aliwatesa sana na kuwabebesha mizigo ya dhambi wanadamu kwa nguvu za giza,lakini mara baada ya ujio wa mwana wa mungu,shetani na nguvu zake za giza hana uwezo wa kututesa tena kwani jina la yesu ndiyo jina lenye nguvu kushinda majina yote.

NI MUONGO
Hapa duniani dhambi imeletwa na shetani ambaye ni mfalme wa nguvu za giza kwani utakumbuka kuwa baada ya mungu kumpatia Adamu msaidizi wake Eva aliwapa sharti moja muhimu ya kwamba wale matunda yote katika bustani aliyowakabidhi isipokuwa tunda la mti wa katikati,shetani(mfalme wa uongo)akamdanganya Eva kuwa endapo watakula tunda kutoka katika mti wa katikati watakuwa na nguvu sawa na mungu hivyo kwa uongo wa shetani,Adam na Eva wakatenda dhambi.

ANA WIVU
Biblia inasema kuwa upendo,huruma na rehema za mungu kwetu ni za ajabu,pamoja na kwamba sisi hatutambui upendo na huruma aliyonayo mungu juu yetu haimaanishi kuwa atatuacha, ndiyo maana alimtoa mwanae wa pekee ili atukomboe,ni upendo wa ajabu kwani sisi ndiyo wakosaji lakini bado mungu ametupa msamaha bure kwa wote watakao amini jina la yesu.Shetani anajua ukweli huu na ana wivu juu ya upendo huu wa muumba kwetu ndiyo maana halali anakesha kutugombanisha na mungu.

NI MSALITI
Katika mpango huu mwema wa mungu,shetani huyuhuyu alikuwa ni mshirika,tena mmoja kati ya washirika wa juu lakini kwa tamaa ya madaraka na wivu,akamsaliti mwenyezi mungu,hata anapowatumia wanadamu hujidhihirisha kama mtu mwenye kusahau fadhila na kuwasaliti watu wake wa muhimu,unajua kila kitu kuhusu Yuda kwani pamoja na kuwa mwanafunzi wa yesu kwa takribani miaka mitatu wakitembea huku na kule akiona miujiza yote aliyokuwa akitenda kristu na kuthibitisha kuwa yeye ndiye massiah,lakini shetani alimshawishi hadi akamsaliti mwana wa mungu kwa vipande thelathini vya sarafu.

NI MUOGA
Katika safari zake yesu akiwa na wanafunzi wake popote walipokwenda,kwa kujua uwezo wake watu wenye matatizo mbalimbali walimfuata aweze kuwafungua na kuwaponya toka katika kifungo cha huyu mfalme wa uongo aliyewatupia mapepo na magonjwa sugu wafungwa hawa wa shetani mara walipokuwa wakihisi uwepo wa mtakatifu mwana wa mungu na mfalme wa amani,pepo hao walilia kwa uoga na kuhamaki hata kumuomba bwana awaruhusu wawaingie wanyama na kutoweka mara moja.

ANA CHUKI
Katika kizazi chote cha mwanadamu kilio,mateso,maumivu na vikwazo vimekuwa ndiyo njia na mbinu ya mwovu huyu kutufanya tusifurahie na kutambua upendo na huruma ya muumba wetu,ni kwa sababu shetani ana chuki dhidi yetu sisi wanadamu,hututupia mapepo,hutufanya tuwe na tamaa,wasiwasi na hofu juu ya dhambi zetu kitu ambacho mungu kwa huruma na rehema zake ametupa msamaha na kuzitupilia mbali dhambi zetu.

ANATUMIA NGUVU ZA GIZA
Shetani hututisha kwamba anaweza kutudhuru au kutukwamishia baraka na neema zetu zitokazo kwa mungu,lakini nakuhakikishia mkristu mwenzangu shetani hana nguvu zozote bali ni muongo na matendo yake yote ni matendo ya nguvu za giza na kwamba nguvu zetu sisi ni kubwa kuliko zake kwani mara atakapotukabili tu,tunampambanisha na mfalme wa nguvu za mwangani yesu kristu ambaye jina lake lapita majina yote.

ATATUPWA JEHANAMU
Maandiko matakatifu yanasema kwa wale ambao hawatamtii mungu na kuheshimu amri zake kwa kupenda mambo ya kupita katika hii dunia kwa kumfuata shetani,wao pamoja na kiongozi wao wote watatupwa jehanamu katika moto wa milelele sehemu ambayo maandiko yanasema itakuwa ni kulia na kusaga meno.


NGUVU ZA YESU KRISTU
Wapo wanadamu waliodanganyika kwa kuamua kumfuata shetani na nguvu zake za giza wakidhani kuwa atawatatulia matatizo yao pasipo kujua kuwa wanajiweka katika hatari ya kisasi cha mungu kuwa juu yao,nakushauri mwanadamu mwenzangu chukua uamuzi sahihi sasa kwa kumwamini na kumfuata yesu kristu kwani ana MAMLAKA duniani na mbinguni pia,ana NGUVU kushinda shetani kwani amekabidhiwa na mungu mwenyezi, ni KWELI kwani yesu kristu ni neno la mungu lililo hai,ahadi yake ya kuja kutuchukua ni ya kweli na ataitimiza kwani ni MWAMINIFU,alipoagizwa na mungu kuja kutukomboa sisi wanadamu alimkabili shetani na kuishinda dhambi pale kalvari kwani ni JASIRI,popote alipokwenda alikuwa akiwafungua na kuwaponya watu waliokuwa wamefungwa na kuteswa na shetani kwani kristu ana UPENDO wa kweli juu yetu,miujiza yake yote anayotenda ni mungu hutenda kwa NGUVU ZA MUNGU kwani hivi sasa YUKO MBINGUNI  ameketi kuume kwa mungu baba na atakuja kutuchukua mimi na wewe.