LUKA 15;11-24
"Kulikuwa na mtu mmoja mwenye wana wawili. Yule mdogo, alimwambia baba yake: Baba, nipe urithi wangu. Naye akawagawia mali yake. Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo. Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika. Akaomba kazi kwa mwananchi mtu mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe. Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu. Alipoanza kupata akili akafikiri: Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa? Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako. Basi,
akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba
yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na
kumbusu. Mwanawe akamwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao. Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu! Mchinjeni ndama mnono; tule kusherehekea! Kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa, kumbe yu mzima alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana. Wakaanza kufanya sherehe".
Yesu alitoa fumbo hilo hapo juu kwa lengo la kuonesha upendo alionao Mungu baba kwetu sisi wanadamu na kwamba Mungu anatupenda lakini anachukia dhambi zetu. Mafarisayo na walimu wa Sheria walinung'unika hata kudiriki kusema "Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao." Baada ya kuwaona Wahalifu na Watoza ushuru wakimsikiliza Yesu, hivyo katika fumbo hili Yesu kama kawaida yake kutumia mafumbo kuelezea upendo,huruma na rehema za Mungu kwa Mwanadamu alikuwa ana maana ifuatayo.
Mtu mmoja mwenye wana wawili;
Katika fumbo lake Mwokozi wetu yesu kristu kwa wale Wahalifu na Watoza ushuru alitumia "mtu mmoja mwenye wana wawili" akimaanisha Mungu ambaye ana wana wawili ambao ni mmoja mkubwa ambaye hutii na kufuata mapenzi ya baba yake na wapili mdogo ambaye kwa tamaa hupotoka na kufuata anasa za kupita za hii dunia.
Mwana Mkubwa na Mdogo;
Katika maana ya kiroho,Yesu alipotumia neno mwana mkubwa alikuwa anamaanisha wanadamu ambao humpenda,kumtii na kutimiza mapenzi ya Muumba wao.Kwa upande wa pili alimtumia mwana mdogo kuonesha wanadamu ambao kwa tamaa zao za kimwili huamua kumkosea muumba wao.
Urithi;
Katika maisha yetu ya kimwili hivi leo,mzazi au mlezi humwandalia mwanae mali na pesa kama urithi, lakini katika fumbo lake kristu urithi kutoka kwa Mungu si mali wala pesa bali ni matunda ya kiroho ambayo ni muhimu sana katika maisha yetu,nayo ni furaha,amani,upendo,ukarimu,matumaini na imani. Urithi huu wa thamani hupatikana tu kwa kumwamini na kumtegemea Yesu kristu tukiwa hapa duniani na Mungu ameahidi kutupa urithi huu tutakapofika katika makazi yetu ya milele mbinguni.
Baba,nipe urithi wangu;
Hii ni kauli ya mwana mdogo,ambaye Kristu alimtumia katika fumbo hili kusawiri wanadamu ambao kwa tamaa za kimwili huamua kumkosea Mungu na hapa unamwona mwana huyu akiomba urithi,si mali wala pesa kama kristu alivyomaanisha mwana huyu alikuwa anaomba furaha,amani,upendo,ukarimu,matumaini na imani ambapo kimsingi hakuwa na uwezo wa kuumudu,kifupi mwana huyu mpotevu alitaka kuendesha maisha yake kwa tamaa zake akitegemea kuishi kwa furaha,amani,upendo,ukarimu,matumaini na imani kitu ambacho bila Yesu hakiwezekani.
Naye baba akamwagia mali yake;
Mungu alipotuumba sisi wanadamu alitupa uhuru wa kuchagua kumpenda au kutokumpenda vile kumtii au kutokumtii kwani upendo na utii wetu utakuwa wa thamani kama ni wa hiari yetu wenyewe japo angeweza kutuumba wote tumpende na kumtii lakini hii isingethibitisha upendo wa dhati.Katika fumbo hili mwana mpotevu alipoomba urithi wake,baba naye akamwagia mali yake...Hapa Yesu ana maanisha kuwa mtu yeyote ambaye kwa hiari yake ataamua kutompenda na kumtii mungu chaguo ni lake haitachukua muda mrefu kujuta kama ilivyokuwa kwa mwana mpotevu.
Aliuza urithi wake;
Utaona kwamba urithi aliopewa mwana huyu si pesa bali alipoupata ndipo akaamua kuuza ili apate pesa.Mungu alijua wazi kuwa wanadamu tutahitaji pesa na pesa ilikuwa muhimu enzi hizo hata leo pia,Pesa kama pesa si dhambi bali jinsi ya kuipata au kuitumia ndipo huzaliwa dhambi ambayo mshahara wake ni mauti.Katika fumbo hili Yesu anaonesha namna ambavyo mwana mpotevu aliweka rehani urithi wake wa thamani ambao ni furaha,amani,upendo,ukarimu,tumaini na imani ilimradi apate pesa atakayotumia kukidhi tamaa zake na anasa zakupita za hii dunia.
Akaenda nchi ya mbali,akatumia hovyo;
Baada ya kuuza urithi wake na kupata pesa,mwana mpotevu alisafiri na kwenda nchi ya mbali,Akizungumza mbele ya Wahalifu na Watoza ushuru Yesu alitumia neno "nchi ya mbali" hakumaanisha umbali wa maili wala kilomita bali umbali wa kiroho,kwamba mwanadamu anapoamua kufuata tamaa zake na kupinga mapenzi ya Mungu katika maisha yake anakuwa amejitenga yeye mwenyewe na kujiweka mbali na chanzo cha furaha,amani,upendo,ukarimu,matumaini na imani katika maisha yake.
Alimaliza kila kitu,kukatokea njaa kali;
Mali,pesa na vitu vyote katika hii Dunia vinapita tu,ndiyo maana Yesu katika habari ya mwana mpotevu anafundisha kuwa tuwapo hapa Duniani tutambue kila kitu tukionacho kina mwisho wake,pesa na starehe za hii dunia zina mwisho na mshahara wa dhambi ni mauti....Kama ilivyokuwa kwa mwana mpotevu baada ya kumaliza kila kilichowafanya wanadamu kutomtii Mungu njaa kali itafuatia,si njaa ya chakula wala kukosa mali bali ni njaa ya ule urithi waliouuza ili kukidhi haja zao za muda,njaa ya furaha,amani,upendo,ukarimu,matumaini na imani.
Akaanza kuhangaika;
Yesu katika mahubiri yake mara kwa mara alikaririwa akiweka wazi kuwa maisha katika yeye yataambatana na mateso kwani hata yeye aliteswa lakini alijishusha na kukubali kifo cha kikatili kwa kusulubiwa msalabani ili atukomboe sisi wanadamu,lakini kwa wale tunaomwamini Yesu Kristu kama mwokozi na mfalme katika maisha yetu tutapitia mateso kwa furaha,amani,upendo,ukarimu,matumaini na imani tukijua Kristu yu pamoja nasi....Kwa wasiomwamini Yesu kama mwana mpotevu huhangaika na wasipate pa kukimbilia.
Alitamani kula chakula cha nguruwe,Hakuna aliiyempa kitu;
Baada ya kuhangaika sana akaomba kazi kwa mwananchi mtu mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe.Katika enzi hizo Nguruwe alichukuliwa kama mnyama haramu hivyo kitendo cha mwana mpotevu kulisha Nguruwe kinasawiri wanadamu ambaye Mungu amemuuumba kwa mfano wake anaposhindwa kumtii Mungu na kufuata tamaa zake hupoteza hazina yake muhimu ya upendo,huruma na neema ya Mungu na kujikuta akigubikwa na kuangamia katika dhambi. Baada ya kupoteza hazina hii hakuna mwanadamu anayeweza kuirejesha,mwana mpotevu pamoja na kutapanya mali akiwa na marafiki wakati wa njaa ulipofika hakuna rafiki hata mmoja aliyejitokeza kumpatia msaada.
Alipoanza kupata akili akafikiri;
Tunapomkufuru Muumba wetu na kufuata tamaa zetu tunakuwa tumepungukiwa akili kwa kiasi fulani,pengine uongo wa shetani umetufumba macho tusitambue neema na huruma aliyonayo mungu kwetu.Mwana mpotevu alipungukiwa akili hata akaingia katika mtego wa mwovu maana alifuata hisia zake,maandiko matakatifu yanasema Hisia ukizifuata mwisho wake ni dhambi,Muumba wetu huruhusu machaguo yetu kwa kiasi fulani lengo likiwa kutuonesha kuwa tukiachwa wenyewe kamwe hatuwezi kufanya maamuzi sahihi kwani hatutambui na wala hatuelewi hata kitu kimoja kijacho,lakini uamuzi ni wetu kutambua kuwa tumetenda kosa pale tunapojikuta maovuni kama Mwana mpotevu alivyopata akili akajiuliza "Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa?" akasema "Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako. Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake".
Alipokuwa yu mbali,baba yake alimwona;
Funzo la Yesu katika hili fumbo ni kwamba wakati wowote tunapochukua uamuzi sahihi wa kumrudia muumba wetu yeye yu nyumbani mwake macho yake ameyaelekeza kwetu,hii ina kwamba tangu wanadamu tunapotenda dhambi hatukomi kuwa wana wa mungu na Mungu anampenda bali anachukia dhambi zake na punde tunapoamua kumrudia na kumwomba msamaha yeye ndiye wa kwanza kutupokea na kutukumbatia kwani msamaha upo tena ni bure kwani Yesu amekwisha lipa dhambi zako na zangu pale kalvari.Kama mwana mpotevu alipoanza kumwambia Baba yake "Nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao".
Lakini Baba yake akawaambia watumishi wake;
"Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu! Mchinjeni ndama mnono; tule kusherehekea! Kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa, kumbe yu mzima alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana. Wakaanza kufanya sherehe"...Kwa kutumia fumbo hili,Yesu Kristu aliwajibu Mafarisayo na Walimu wa sheria kuwa kitendo chake cha kuzungumza na Wahalifu na Watoza ushuru ni mfano wa jinsi gani Mungu anatupenda na amekwisha tusamehe Dhambi zetu kazi ni yangu mimi na wewe kupata akili na kuamua kumrudia na njia pekee ni Yesu Kristu.
LUKA 5;8-5
"Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa
akizipanda, nyingine zilianguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa
angani wakazila.
Nyingine zikaanguka penye mwamba; zilipoanza kumea zikakauka kwa kukosa rutuba.
Nyingine zikaanguka kati ya miiba, na miiba ikamea pamoja nazo ikazisonga.
Nyingine
zikaanguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia. Alipokuwa
akinena hayo alipaza sauti akisema, Mwenye masikio ya kusikia, na
asikie".
Kama ilivyokuwa kawaida yake yesu kristu katika kile ambacho kinafahamika kuwa ni kutuachia mafunzo kupitia kwa wafuasi wake,ili kuwafunua waweze kufikiri kwa kina na kuweza kutambua kwamba ufalme aliokuja kuuanzisha ni wa mbingu wala si wa duniani.Lakini hapa mbele ya mkusanyiko wa watu mbalimbali waliomjia toka katika kila mji wakihitaji kuponywa na kufunguliwa,mwana wa mungu alinena maneno hayo,nasi kutokana na mfano huo tunaweza kupata somo lifuatalo.
Mbegu ni neno la Mungu.
Ili kupata mazao,mkulima ni sharti apande mbegu na mazao yatatokana na mbegu yenyewe,katika mfano huu 'mbegu' aliyoipanda mpanzi ni neno la mungu,ni sheria na utaratibu wa maisha yanayompendeza mungu ulioainishwa wazi katika biblia yake takatifu.
Udongo ni mioyo yetu.
Mbegu ili iweze kuzaa matunda mengi na bora hutegemea sana ubora wa udongo ambao mbegu hiyo hupandwa,vivyo hivyo katika ufalme wa mungu ili neno liweze kufanya kazi yake ipasavyo ni lazima mioyo yetu iwe tayari kulipokea na kuliamini ndipo wokovu wa kweli huchukua nafasi na kubadili maisha yetu toka katika dhambi kwenda katika wokovu.
Wale wa karibu na njia.
kuna watu hubahatika kusikiliza mahubiri au kusoma neno la mungu katika biblia takatifu na kulipokea neno mioyoni mwao na kuanza kuishi maisha matakatifu katika kristu, lakini kabla hawajakua kiroho hupotoshwa na kurejea kuishi katika maisha yao ya uzinzi,ulevi,wizi,usaliti,uchoyo,ubinafsi hata ushirikina kama waliyokuwa wakiishi kabla ya kupokea wokovu wa yesu, hawa
ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka,
Wale wa penye mwamba.
Kuna binadamu ambao katika hatua yao ya mwanzo kabisa kulipokea neno iwe ni kwa njia ya mahubiri,kusoma au pengine kwa njia ya nyimbo za kumsifu bwana faraja ya kristu iliwaingia na kufanyika furaha isiyo kifani ndani yao,lakini baada ya muda mfupi pindi wapambanapo na vikwazo na majaribu mbalimbali kama vile kuteswa,kutengwa,kushindwa,kukataliwa hata kuaibika.neno(mbegu) hukosa mizizi(imani) na kushindwa kumea.hawa ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha;
nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa
hujitenga.
Zilizo anguka penye miiba.
Katika dunia hii ya leo,dunia iliyojaa chuki,wivu,tamaa na usaliti karibu robo nne ya wanadamu wametambua umuhimu wa kulipokea neno na kumwamini yesu kristu kama mwokozi wao,miongoni mwao wamelisikia neno labda kupitia mahubiri,televisheni,biblia,nyimbo za injili au kushiriki misa na matamasha ya kidini lakini kabla neno hilo(mbegu) halijaota mizizi na kuchipua(kukua kiroho) watu hawa wamedanganyika na starehe za kupita za hii dunia kama ulevi,uzinzi na tamaa ya pesa na kujikuta imani yao imetoweka.hawa ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote.
Zile za penye udongo mzuri.
Kama vile ambavyo mbegu huchipua kukua na kuzaa matunda ipandwapo katika udongo mzuri,basi watu hawa wamepata kusikia habari njema na msamaha wa dhambi zao kupitia damu ya yesu kristu iliyomwagika pale msalabani na kuamua kulipokea neno mioyoni mwao,kulishika,kuliamini na kulitenda bila kujali mateso na vikwazo wanavyopambana navyo katika maisha ya imani kama vile kukashifiwa,kuchekwa,kudharauliwa na kudhihakiwa.hawa ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia.
Sisi ni akina nani?
Mpendwa mkristu mwenzangu,kabla masiah hajafafanua mfano huu alinena na kupaza sauti akawaambia wafuasi wake "ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme wa Mungu; bali wengine kwa mifano, ili wakiona wasione, na wakisikia wasielewe".Japo alikuwa akizungumza na wafuasi wake,lakini hii inatuhusu moja kwa moja mimi na wewe ambao kupitia maandiko matakatifu kwa uwezo wa roho mtakatifu tumepata kuujua ukweli juu ya ufalme wa mungu basi tuupoke mioyoni mwetu na tusiwe kama wengine(wasioamwamini yesu) ambao pamoja miujiza,uponyaji na ufufuko wa bwana wetu yesu kristu hawaoni na pamoja na mahubiri,nyimbo na hata maombezi bado hawajafungua mioyo yao na kulipokea neno(mbegu) la mungu ili liweze kukua ndani yao na kufanya waishi maisha yanayompendeza muumba hapa duniani na mbinguni pia.
YOHANA 15;1-7
"Mimi ni mzabibu wa kweli na Baba yangu ndiye mkulima. Kila
tawi ndani yangu lisilozaa matunda, Baba yangu hulikata; na kila tawi
lizaalo, yeye hulisafisha ili lipate kuzaa matunda zaidi. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya mafundisho nili yowapa. Kaeni
ndani yangu nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa
matunda pasipo kuwa sehemu ya mzabibu, vivyo hivyo, ninyi msipokaa ndani
yangu hamwezi kufanya lo lote. Mimi
ni mzabibu; ninyi ni matawi; anayekaa ndani yangu nami ndani yake, huyo
huzaa matunda mengi sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya lo
lote. Mtu asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi na kunyauka. Matawi hayo hukusanywa na kutupwa motoni, yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lo lote mtakalo nanyi mtatendewa".
Haya ni maneno ya mwokozi wetu yesu kristu kwa wanafunzi wake, mwana wa mungu aliwaambia maneno haya katika kipindi cha mwisho akiwaachia usia muhimu wanafunzi wake kabla hajainuliwa, maneno haya ya kristu kwa wanafunzi wake yanatuhusu moja kwa moja sisi kama wafuasi wake na kwamba japo yalitamkwa karne nyingi zilizopita yana maana kubwa leo hivi tunapoishi.
- Baba yangu ndiye mkulima;
mkulima ndiye ambaye mmiliki wa shamba,mimea na mazao pia. katika mstari huu, kristu anamaanisha kuwa baba yake mungu mwenyezi wa mbinguni ndiye mmiliki wa mbingu na dunia hii pia ndiye aliyemleta duniani ili sisi kupitia yeye tukombolewe.
- Mimi ni mzabibu;
mzabibu ni mmea uliopandwa na mkulima katika shamba,katika mstari huu yesu anamanisha kuwa yeye mwenyewe ndiyo mti wa mzabibu ambao mungu baba amemleta duniani ili kupitia yeye tumjue mungu na kutii amri zake vilevile tuweze kukombolewa.
- Ninyi ni matawi;
matawi ni sehemu ya mmea ambayo ndiyo hutoa matunda,hapa mwokozi anamaanisha kwamba,sisi wanadamu ndiyo matawi na kwamba lazima tuwe ndani yake naye ndani yetu ili tuweze kukombolewa,tusipomtegemea yeye hatuwezi tukazaa matunda kwani ili tawi lizalishe matunda sharti liwe ndani ya mti.
- Matunda mengi;
mkulima akipanda mti,matarajio yake ni kuvuna matunda mengi,katika mstari huu kristu anaonyesha kuwa ili matendo yetu yawe mema ni lazima tumtazame, kumuamini na kumfuata yeye mwana wa mungu,kwani ili tawi lizalishe matunda mengi linategemea zaidi mti wenyewe.
- Anayekaa ndani ya kristu;
katika maneno haya mwokozi wetu yesu kristu ana maanisha yeyote aliyetubu dhambi zake na kumpokea yeye kama mwokozi na mfalme katika maisha yake,yule aliyezaliwa upya kiroho na kutii amri za mwenyezi mungu ndiyo anayekaa ndani kristu na yeye ndani yake,mtu(tawi) huyu hutenda kiroho na matendo(matunda) yake mema humpendeza mungu.
- Asiyekaa ndani ya kristu;
mtu asipokaa ndani yake hawezi kufanya lolote,anamaanisha watu ambao hawajaipokea zawadi ya mungu ya wokovu, hawatauona ufalme wa mungu,pamoja na matendo yao mema maandiko yanasema 'yeyote atakayeamini ataishi milele lakini yule asiyeamini kuwa yesu kristu ni mwana wa mungu na alipokwenda msalabani alilipa dhambi zetu zote,huyu hataishi atatupwa nje kama tawi na kunyauka na matawi hayo hukusanywa na kutupwa motoni yakateketea.
- Faida ya kukaa ndani ya kristu;
katika mstari wa saba yesu anasema 'lakini ninyi mtakao kaa ndani yangu na maneno yangu yakakaa ndani yenu' hapa anawalenga wale watakaomwamini na kumfuata,wale ambao neno la mungu litakaa ndani yao anasema kwamba 'ombeni lolote mtakalo nanyi mtatendewa' chochote watakachoomba katika jina lake mungu mwenyezi atajibu maombi yao,kumbuka maombi yataendana na mapenzi yake.
ZABURI 23;4
"Japo napita katika bonde la mauti,sitaogopa mabaya Bwana yu pamoja nami,gongo lake na fimbo yake Bwana vyanifariji"
GONGO
Ni fimbo ambayo ina kamba ya ngozi kwa mbele yake,hii ni siraha maalum kwa ajili ya kuwakokota mifugo pale ambapo wanakuwa wamekwama katika mabonde(vikwazo)
FIMBO
Ni siraha itokanayo na mti na ambayo hutumiwa na mchunga mifugo na kazi yake kuu ni kuwalinda mifugo dhidi ya wanyama hatarishi(maadui)
Wakati nabii Daudi anaandika Zaburi hizi,alikuwa anapita katika wakati mgumu sana katika maisha yake,kuvamiwa kwa mji wake pamoja na vifo, utekaji wa wafuasi wake na mali zao, upinzani, vitisho vya kuangamizwa pamoja na majaribu mengi ya kiroho ni mfano tu wa magumu abayo nabii Daudi alikuwa anapambana nayo katika mapito yake......Maandiko yanasema pamoja na magumu hayo, Nabii alielekeza jicho lake na kumtazama mungu kwa imani akijua Mungu kwa kutumia gongo lake angemkokota na kumkwamua toka katika vikwazo na upinzani aliokuwa akikabiliana nao,vilevile nabii Daudi aliamini kuwa mungu kwa kutumia fimbo yake atamlinda dhidi ya maadui waliokuwa wakihatarisha uhai wake.
Tujikabidhi kwa mungu:tumwamini na kumkabidhi maisha yetu na kila kitu kinachohusu maisha yetu hapa duniani na mbinguni pia tukiwa na tumaini moja kuwa atajitukuza kupitia maisha yetu.
Tumwamini mungu:yatupasa kuwa na imani kwamba mungu atageuza mapito yetu(vikwazo na maadui) na kuwa mema kwetu.
Tupokee busara,upendo na baraka zake:kama wafuasi wa kristu kitu cha muhimu ni kumpa mungu nafasi ili ajitukuze kupitia maisha yetu.
Tumshukuru mungu:pamoja na vikwazo na magumu tunayopitia katika misha yetu yatupasa tumshukuru mungu kwani tupitapo katika haya tunajifunza mambo mengi makuu ya mungu na kwamba ana lengo maalum alilolikusudia hata akatupitisha katika vikwazo na magumu.
Kama ilivyokuwa katika maisha ya nabii Daudi,hata katika maisha yetu vikwazo na maadui HAVIEPUKIKI,vilikuwepo
jana,vipo leo na kama havipo basi karibuni au hata baadae tutakabiliana
navyo.......Pia pamoja na kwamba sisi wanadamu ndiyo tunaoweza
kusababisha vikwazo au kuvutia maadui kwa vitendo vyetu sisi
wenyewe,ukweli ni kwamba mungu ndiye HUPANGA KIWANGO
cha maadui na vikwazo vitakavyo tukabili kwani anatufahamu na kamwe
hataruhusu tujaribiwe zaidi ya viwango vyetu pia katika kila jaribu
atatupatia uwezo kulishinda.......muhimu kuliko vyote mungu anatupenda
na kutujali na angependa kutufundisha juu ya upendo,ulinzi na baraka
zake na ukweli ni kwamba TUNAJIFUNZA ZAIDI tuwapo katika vikwazo na maadui wakitukabili.
TUFARIJIKE
Kama hali ilivyokuwa kwa nabii Daudi,na sisi kama wana wa mungu,tuliompokea yesu kristu mwokozi na mfalme wa maisha yetu tunayo faraja kubwa ndani ya mioyo yetu kwani GONGO la mungu latosha kutuvusha na kutukwamua kutoka katika kila aina ya shida na vikwazo katika maisha yetu iwe ni magonjwa,umasikini,vita hata kutengwa.......kwa kutumia FIMBO yake iliyo tukuka atatulinda dhidi ya maadui wa kila aina iwe ni wasaliti,wachawi,wezi,wanafiki hata wachochezi katika maisha yetu.
MATHAYO 5;13-16
"Nyiyi ni chumvi katika dunia,hivyo chumvi ikikosa ladha itawezaje kutumika? ni sawa na uzuri pasipo faida bali hutupwa na kukanyagwa na miguu ya wanadamu. Ninyi ni mwanga katika dunia,mji ulioinuliwa kilimani kamwe haufichiki. Wala taa haiwashwi halafu ikafunikwa ndani ya kikapu bali huinuliwa katika ngazi yake na hutoa mwanga kwa watu wote walio ndani ya nyumba. Mwanga wenu ung'are kwa watu wote ili waone mema yenu wamtukuze mungu aliye mbinguni"
hayo ni maandiko kutoka katika biblia ambapo ukisoma katika kitabu cha mathayo utaona kwamba Yesu kristu baada ya kundi kubwa la watu kutoka Galilaya,Decapolis,Yerusalem na yudea lilipokua likimfuata ili kupata mafunzo aliamua kutafuta mapumziko katika kilima na mara baada ya kuketi kama kawaida yao wanafunzi wake walimwendea na hapo akafumbua mdomo wake na kuwafundisha akisema maneno hayo.Mafunzo hayo yalikuwa muhimu sana kwa wanafunzi wake pia ni muhimu sana kwetu hivi leo,hebu tazama bwana alikuwa anamaanisha nini aliposema.
NINYI NI CHUMVI KATIKA JAMII
Chumvi hutunza,katika miaka ya nyuma chumvi ilitumika kutunza vyakula kama nyama na samaki ili isiharibike,chumvi ilikua muhimu kama ilivyo friji katika miaka hii....Hapa kristu anatufundisha maisha yetu kama wanafunzi wake yanapaswa kuwa ya mfano na ushawishi kwa jamii ili jamii ipokee ufalme wa mbingu.
Chumvi huleta mabadiliko,hubadili ladha ya chakula mara tu inapochanganyika katika chakula husika hivyo nasi pia kama wakristu maisha yetu yanapaswa kuleta mabadiliko tuwe tumeelimika au la,tuwe matajiri au masikini inawezekana tukiwa na yesu ndani yetu kubadili mienendo ya watu na wakamfuata yesu.
Chumvi ina ladha,ikiingia katika chakula kinakuwa na ladha ya chumvi,hapa kristu anatufundisha kwamba pamoja na tamaa,chuki,wivu,uchoyo,usaliti,mapigano na hata mauaji yaliyoenea katika jamii ya sasa tukimruhusu roho mtakatifu aishi maisha ya kristu kupitia sisi jamii itakuwa na ladha kama yetu sisi ambao ni chumvi.
Chumvi huleta kiu,tazama maisha katika jamii yetu kila mtu anahamaki,kuteseka na kutapatapa na mizigo ya dhambi iwe ni rushwa,tamaa,anasa,pombe na dawa zakulevya mradi ni dhambi lazima inamtesa,hivyo sisi tuliompokea yesu kristu kama mwokozi na mfalme wetu tunapoishi maisha ya furaha na amani inawapa kiu walioko katika gereza la dhambi nao watubu dhambi zao na kumpokea yesu.
Chumvi huenea,iko wazi kwamba chumvi kidogo sana inaweza kuleta ladha katika chungu kikubwa tu,hivyo ndivyo injili hufanya kazi,habari za yesu zilianza na kikundi kidogo tu cha watu na kuenea dunia nzima,hivyo na sisi tusife moyo kuishi maisha katika bwana tukiamini kuwa kazi yetu ni kubwa na mwisho wake ni wokovu.
Chumvi hupoteza ladha yake,bwana yesu alisema "kama chumvi ikipoteza ladha yake,haifai tena kwa chochote"japo chumvi haiwezi ikapoteza ladha yake lakini wakati ule chumvi ilitokana na kuanika maji na mchanga wa baharini hivyo ule mchanga ulioshindwa kuganda na kuwa chumvi iliokamilifu ulikuwa unatupwa, katika mtazamo huu huu waumini ambao huendekeza dhambi katika maisha yao hupoteza ushawishi wa kuleta mabadiliko katika jamii yao.
NINYI NI MWANGA KATIKA JAMII.
Mwanga hutoka kwa yesu,yesu aliwaambia wanafunzi wake kuwa wao ni mwanga katika dunia kwa maana kwamba kadri ambavyo wangeishi kwa kufuata mafundisho yake mwanga wao ungekuwa mng'avu zaidi na zaidi ndiyo maana dunia nzima leo pamoja na elimu na maendeleo yote haya tunajifunza maandiko ambayo mengi yake yaliandikwa na wavuvi.
Mwanga huelekeza njia,kama ambavyo taa huongoza meli majini vivo hivyo pia mwanga humulika njia,maisha ndani ya yesu ni maisha yenye furaha na amani kwani bwana ndiye mchungaji wetu tumwogope nani?dunia hii ina mamia ya watu ambao wapo tayari kumpokea yesu endapo tu watahubiriwa injili hivyo sisi kama waumini tuwaelekeze na tumwombe mungu atujaalie uwezo ili tushirikishe wenzetu katika mpango wa wokovu.
Mwanga huonesha,mwanga mdogo kama mshumaa unaweza kung'arisha chumba kikubwa,hivyo si lazima uwe mtu mwenye upako wa ajabu kupindukia ili uweze kuwaelezea watu juu ya habari ya yesu kristu na wokovu kitu kitakachofanya mwanga wako ung'are ni matendo yako hivyo mkristu mwenzangu hakikisha huendekezi dhambi katika maisha yako.
Mwanga huzimika,katika taa ya chemli utambi lazima upandishwe ili kupata moto mkubwa pia kioo kikiwa safi mwanga utasambaa umbali mkubwa..lakini utambi ukiwa mrefu sana na kioo kikawa kichafu mwanga hautafikia umbali mpana ...mkristu mwenzangu,dhambi inapoingia katika maisha yako ni kama uchafu unapoingia katika kioo cha taa, lakini unapomfuata na kumwamini yesu kristu hutazuia mwanga wake kung'ara kupitia wewe.
JE,WEWE NI NANI?
Mwanga katika jamii yako? ushawishi katika jamii yako unapungua? mwenendo wako,matendo yako,sifa yako na maongezi yako yanawasogeza watu kwa yesu au yanawaweka mbali na mwana wa mungu? Mpendwa, mimi na wewe tunao wajibu mkubwa wa kuwaleta wanadamu katika wokovu wa yesu kristu kupitia roho mtakatifu,namuomba mungu akuondolee kipingamizi chochote kinachokuzuia usiwafikie watu na kuwapa habari njema za wokovu,mruhusu mungu aongee kupitia moyo wako na ushinde kila aina ya dhambi kwani mimi na wewe tunapoishi maisha mema katika yesu tunakuwa CHUMVI na MWANGA katika jamii.
Mwanga katika jamii yako? ushawishi katika jamii yako unapungua? mwenendo wako,matendo yako,sifa yako na maongezi yako yanawasogeza watu kwa yesu au yanawaweka mbali na mwana wa mungu? Mpendwa, mimi na wewe tunao wajibu mkubwa wa kuwaleta wanadamu katika wokovu wa yesu kristu kupitia roho mtakatifu,namuomba mungu akuondolee kipingamizi chochote kinachokuzuia usiwafikie watu na kuwapa habari njema za wokovu,mruhusu mungu aongee kupitia moyo wako na ushinde kila aina ya dhambi kwani mimi na wewe tunapoishi maisha mema katika yesu tunakuwa CHUMVI na MWANGA katika jamii.