Thursday, November 1, 2012

JIRANI YANGU NI NANI HASA?

Katika kile kinachoaminika kuwa ni kutafuta chanzo  ili wapate sababu na misingi ya kuweza kujitetea kwa kumkana mwana wa mungu,Wayahudi walikuwa wakimuuliza maswali ya mtego bwana wetu Yesu kristu, pasipo kujua kwamba Yesu alikuwa anatambua mawazo yao kabla hata hawajazungumza chochote, pia  kwa kudhani kuwa walikuwa wakimuuliza maswali ya mitego, kumbe walikuwa wakidhihirisha kuwa hawakua na uelewa juu ya mambo ya kiroho, bali shetani alikuwa akiwatumia kukwamisha mpango wa mungu, kupotosha jamii na kugeuza dini ya mungu kuwa njia ya kutimiza matakwa na maslahi yao binafsi



Hivyo katika kile walichoamini wao ni kutaka kumtega ili waweze kupata sababu za kumhukumu yesu kristu,siku moja akiwa anafundisha neno la mungu,wanafunzi, wafuasi pamoja na kundi kubwa la watu kutoka sehemu mbali mbali waliokuja kwa nia ya kufunguliwa na kupata suluhisho juu ya matatizo yao, alijijitokeza mwanasheria mmoja miongoni mwa mafarisayo waliokuwa wakimpinga mwana wa mungu na kumuuliza swali, mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo.



Mwanasheria; Je,nitafanya nini ili nipate kuuona ufalme wa mungu?


Yesu;  Mpende bwana mungu wako,kwa moyo wako wote,kwa akili zako  zote na kwa uwezo wako wote, utapata kuuona ufalme wa mungu

Mwanasheria; Nimekuwa nikifanya hivyo maisha yangu yote, nitende kipi cha ziada?
       
 
Yesu; Basi mpende jirani yako,kama unavyojipenda.


Mwanasheria; Jirani yangu ni nani hasa?



Hapa ndipo mwana wa mungu alipotumia mfano wa kweli na hakika ili kuweka wazi juu ya utata wa nani hasa ni jirani kwa enzi zile hata katika maisha yetu hivi leo, akaanza kwa kusema.



"Mtu mmoja mwenyeji wa Yerusalem alikuwa akisafiri kwenda katika mji wa Judea,alipofika katika lango kuu maeneo ya Yeriko,watekaji nyara walimvamia,wakampora kila alichokuwa nacho na kumjeruhi vibaya kisha wakaondoka zao na kumwacha mahututi. Muda mfupi baadae akapita mtumishi wa mungu, alipomwona majeruhi yule alimtazama akapita pembeni na kwenda zake akielekea hekaruni,baada ya muda si mrefu tena akapita mzee wa kanisa naye akamtazama mtu yule aliyekuwa mahututi  na kupita pembeni kisha akaenda zake pia akiwahi katika nyumba ya ibaada....Baada ya kitambo kirefu kidogo,mtu mmoja mwenyeji wa Samaria akiwa safirini kuelekea nchi ya mbali kupitia Yerusalem alipofika katika eneo la tukio na kumkuta majeruhi yule yu mahututi hajitambui,aliteremka katika farasi wake akambeba majeruhi yule na kwenda nae katika sehemu ya kupumzikia wageni akamkanda majeraha yake kwa maji ya moto na kumpaka mafuta, akampatia tiba madhubuti hata akapata fahamu na kujitambua,  kisha akamlipa mwenye nyumba ile ya kupumzikia wageni na kumwambia "mhudumie mgonjwa huyu na nirejeapo toka safarini nitalipia gharama zote ,kisha akaenda zake,aliporejea kutoka safarini alilipa gharama zote".



Kutoka katika habari hii,iliyopo katika Biblia takatifu katika kitabu cha mtakatifu Mathayo,utaona kwamba kulikuwa na hali ya uadui mkubwa sana kati ya Israel na Samaria kwa ajili ya Wayahudi kuamini kuwa wao ni taifa teule la mungu na mtu yeyote asiye na asili ya Israel hasa wa Samaria alionekana hana thamani machoni mwao na mungu wao pia......Lakini wao wenyewe wameshindwa kutambua thamani na umuhimu wa ndugu na Myahudi mwenzao aliyekua amevamiwa na kujeruhiwa vibaya na kumpita kwa haraka ya kufika katika nyumba za ibaada na kusahau kutoa msaada kwa kiumbe wa mungu ambaye wanamsujudu.....pengine walitawaliwa na hofu ya kuvamiwa pale au kuhusishwa na tukio hilo,tofauti na Msamaria aliyeamua kutoa msaada kwa majeruhi yule bila kujali itikadi,utaifa, wala hofu ya kutekwa na kuhusihwa na tukio hilo......


Baada ya kumaliza kusimulia habari hiyo ambayo ndiyo chanzo halisi cha neno maarufu ambalo hadi leo hii tunalitumia "msamaria mwema",Yesu akamuuliza mwanasheria yule.


Yesu; Je,kati ya hawa watatu nani ni jirani ya mtu huyu aliyekuwa mahututi....?


Mwanasheria; Yule Msamaria...


Yesu; Basi na wewe tenda kama Msamaria huyu na utapata kuuona ufalme wa mungu..

Nasi katika maisha tunayoishi leo,ni muhimu kutambua kwamba,si kwa nafasi,wadhifa au vyeo katika dini au jamii tunayoishi na wala si kwa kumpenda mungu wetu, kwa mioyo yetu yote, kwa akili zetu zote na uwezo wetu wote tu, bali kwa kumpenda jirani yetu pia, kama Msamaria mwema alivyofanya, tukikumbuka kuwa hatuwezi kumpenda mungu tusiyemuona pasipo kumpenda binadamu mwenzetu tunayemuona.