Saturday, October 6, 2012

ZUNGUMZA NA MUNGU

Mungu ni mwema,tena ni mwaminifu,ana upendo mkubwa sana kwetu,huruma na rehema zake hazina mfano, fadhili zake ni za milele na uweza wake hauelezeki kwani kwake hakuna lisilowezekana,ametuumba kwa mfano wake na alipotuumba akatupa utaratibu wa kuufuata katika maisha yetu hapa duniani ili ajitukuze na baadae atushirikishe katika maisha ya milele huko mbinguni.

Katika historia ya mwanadamu,mwenyezi Mungu amekuwa akiwasiliana nasi kwa njia mbalimbali kama vile matendo,ishara au viashiria tofauti na hali ilivyokuwa kwa Adam binadam wa kwanza ambaye kabla hajamkufuru Mungu alikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja yaani aliweza kuiona sura ya Mungu na kusikia sauti yake.baada ya Adam kumkufuru Mungu hakuweza kuiona tena sura wala kuisikia sauti badala yake Mungu alitumia manabii,mitume na watakatifu kuwasiliana na wanadamu.


NENO LA MUNGU
Biblia ni neno kutoka kwa Mungu kuja kwetu wanadamu kupitia manabii,mitume na watakatifu ambao Mungu aliwajaza upako ili waweze kuelezea asili, hisia, mtazamo, mpango wa Mungu juu yetu wanadamu pamoja na ujio wa mwanae yesu kristu,neno la Mungu ni kweli hakika mbingu na nchi vitapita lakini neno litasimama daima.Katika neno lake Mungu ametupa maagizo namna ya kuishi na kumpendeza yeye aliyetuumba.


Mpendwa mkristu mwenzangu,ni vizuri kukumbuka kuwa tunaweza kuzungumza na Mungu kwa namna mbili tofauti na kuzungumza bila imani, katika uzungumzaji wa namna hii watu tunasoma neno, tunafanya maombi, sikiliza mahubiri na kuyaacha hapo hapo bila kujifunza chochote,hali ni tofauti na kuzungumza kwa imani ambapo tunatakiwa kusikiliza  na kusoma neno, kufanya maombi, kulitafakari, kuamini na kulifanya neno kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku.Wakati wote tukizungumza na Mungu kwa imani ni muhimu kutenda haya yafuatayo.

KUTAFAKARI
Wakati tunazungumza na  Mungu iwe ni kwa kusoma au kusikiliza neno lake ni muhimu sana kutafakari juu ya maana ya maandiko husika na nini yanamaanisha ikiwa ni pamoja na kugundua namna ambavyo tutafanya maandiko hayo kuwa sehemu ya maisha yetu.

KUOMBA
Biblia haisomwi kama vitabu vingine vyote,ni muhimu kabla ya kuisoma tumwombe Mungu atuwezeshe kusoma na kuelewa pia atuongoze katika maandiko yanayohusu hali tunayopitia katika kipindi husika katika maisha yetu ili kupitia neno lake azungumze nasi na kutusaidia kupata ufumbuzi wa suala husika.

KUNYENYEKEA
Tunapokuwa tunazungumza na Mungu iwe kwa kusoma,kusikiliza hata kwa sala na maombi ni muhimu kuwa wanyenyekevu, maana yake ni kuwa tunapoomba hatuombi kikaidi na tunapomwomba tukitegemea atatujibu maombi yetu kama mapenzi yake yalivyo.

KUTUMAINI
Ahadi za mungu tunazozisoma katika neno lake au kusikiliza kupitia kwa watumishi wake hakika ni za kweli na wakati ukitimia mungu atatenda, hivyo tuwapo katika maombi tunatumaini kuwa kwa wakati wake mungu baba atajibu maombi yetu.

KUWA NA SUBIRA
Katika historia ya mwanadamu,maandiko yanaonyesha namna mungu alivyokuwa anatenda miujiza na kujibu maombi kwa watu wake, lakini majibu ya maombi hayo hayakuja kama mvua ni kipindi kirefu kinahitajika pengine mungu huwa na maeneo ambayo anayafanyia marekebisho au kutaka kurekebisha wasifu wetu ili baraka zake zitufae zaidi,hivyo subira ni sifa muhimu sana kwetu sisi kama wakristu.

ZUNGUMZA NA MUNGU LEO
Mpendwa,umeshatambua kuwa Mungu anahitaji kuzungumza na wewe leo juu ya maisha yako hapa duniani na mbinguni pia? kama hujatambua, chukua uamuzi sahihi sasa kwa KUSOMA neno lake lililo katika biblia takatifu, pia ili uweze kukua kiroho ni muhimu kwa KUSIKILIZA mahubiri, hivyo tafuta kanisa jirani yako ambalo yesu kristu ndiyo mwokozi na mfalme na ujiunge, kwa kujumuika na wakristu wenzako utazidi KUAMINI na kupitia imani yako ndiyo utazidi kuuona mkono wa Mungu ukitenda miujiza katika maisha yako na wewe utazidi KULITENDA neno..