Monday, January 14, 2013

BWANA, TUOKOE, TUNAANGAMIA!!

Akiwa ufukweni mwa bahari ya Galilaya,kristu aliendelea kuhubiri injili na kutangaza ufalme wake,umati mkubwa ulikuwa mahali hapo ukitaka kuendelea kusikiliza ujumbe mzuri na wenye kufariji uliokuwa ukitoka katika kinywa cha Bwana, Yesu alikuwa akifafanua mafumbo aliyotumia kuuelezea ufalme wa mbinguni aliokuwa amekuja kuuanzisha,akitumia "habari ya mpazi",pia akiufananisha ufalme wa mbingu kama "mbegu ya aladali" na vilevile fumbo la "nyavu za kuvulia samaki".

Baada ya shughuli hii pevu ambayo bwana aliifanya kwa kipindi kirefu pasipo kula wala kunywa aliamua kuuondosha umati huo uliokuwa ukimsikiliza nakutafuta mahali ambapo angepata pumziko,Yesu aliwaamuru wanafunzi wake wapande mashua na kuelekea ng'ambo ya pili ya bahari katika mji wa Genesareti,mji ambao kristu aliendesha shughuli zake bila upinzani mkubwa hivyo aliamini angeweza kujipumzisha vizuri bila usumbufu wowote,katika kupanda mashua,idadi kubwa ya umati bado ilikuwa ufukweni pale na wakati wafuasi wa Yesu wakipanda mashua,watu waliokuwa wakitaka kuendelea kumsikiliza Kristu nao walipanda mashua yao kwani palikuwa na mashua zingine zilizokuwa zikitumika kwa shughuli ya uvuvi na punde safari ikaanza.

Kutokana na uchovu mkubwa pamoja na njaa,kwani kwa siku nzima Yesu alikuwa akihubiri injili pasipo kutia kitu chochote kinywani mwake,mara baada ya kupanda mashua jioni ile aliamua kutafuta mahali tulivu akajipumzisha na usingizi ukampitia.

Kitambo kidogo baada ya safari kuanza jua lilizama, ghafla giza nene likatanda mawinguni,ngurumo kali na radi zikaanza kupiga,upepo kutoka milimani na kimbunga cha ajabu kilianza,mawimbi yalianza kuzipiga mashua walizokuwa wakisafiria.....Miongoni mwa wafuasi wa yesu na umati uliokwa katika mashua zingine pia walikuwa ni watu waliokuwa wakifanya shughuli za uvuvi kwa karibu maisha yao yote,hivyo waliamini hali ile ni ya kawaida na kwamba baada ya muda mfupi bahari ingetulia kama mwanzo,lakini kadri muda ulivyokwenda hali ilizidi kuwa mbaya na mawimbi yalikuwa yakizipiga mashua nazo zikaanza kujaa maji.

Wafuasi pamoja na umati wa wtu katika mashua zile walijaribu kutumia uzoefu wao wa muda mrefu kukabiliana na hali ya hewa wakisahau ni nani aliyewaamuru kupanda katika mashua na kuelekea ng'ambo ya pili,baada ya kufanya jitihada zote na kushindwa maisha yao yalikuwa mashakani kwani mashua zilijaa maji na kuanza kuzama ghafla wakakumbuka kuwa ndani ya mashua alikuwamo aliyeshinda nguvu za mwovu,aliyekemea na kutoa mapepo hata kufufua wafu ndipo hapo wakaamua kumlilia wakiita kwa sauti..


Wafuasi/umati;  "Bwana,bwana...."Tunaangamia na wewe hutujali!!!!!"


Kwa kipindi hicho chote cha dhoruba baharini,Yesu alikuwa amelala usingizi,wafuasi wake walimtafuta lakini kutokana na giza na mahali alipokuwa amelala haikuwa rahisi kupatikana,mpaka mwanga mkali wa radi ulipo mulika ndipo walipomwona mwana wa Mungu amepumzika,ishara ya amani na upako wa Mungu vikidhirika katika usoni pake wakamwendea na kumwamsha wakimlilia kwa kutahamaki wakisema...

Wafuasi/umati;  "Bwana, tuokoe, tunaangamia!!!!!".


Kelele na vilio vya wafuasi na umati wa watu katika mashua zote zilimwamsha Bwana Yesu,kwani mawimbi yalizisogeza karibu mashua hizo hivyo kupelekea vilio na kelele za watu wenye hitaji la kuokolewa kusikika,mara Yesu akaamka na kusimama katikati ya wafuasi wake kisha akawaambia.

Yesu;  "Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba?"

Yesu alipoamka hakuwa na woga katika mwonekano wala maneno yake na wakati akizungumza maneno hayo,bado kelele na vilio viliendelea kusikika na kudhihirisha uhaba wa imani kwa watu wale,Mara Yesu akaondoka, akazikemea pepo na bahari kwa kunyoosha mkono wake wa kuume juu akasema.

Yesu;  "Amani,kuwe shwari"

Ghafla kukawa shwari kuu,mawingu yalisambaa,mwezi ukachomoza,nyota zikang'ara na giza likatoweka,upepo ukatulia,ngurumo zikanyamaza,radi, kimbunga vikakoma na mawimbi yakatulia bahari ikawa shwari,Wafuasi na umati wa watu wakamaka wakisema.

Wafuasi/umati;  "Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?"


Je, ni mara ngapi hali kama hii hututokea? kama ilivyokuwa pale baharini,giza linapotanda katika maisha yetu(sintofahamu),kimbunga cha maisha kinapoanza (majaribu),ngurumo na radi za maisha zinapotukabili (vitisho) na mawimbi yanapotuyumbisha (misukosuko) nasi kama watu wale hujaribu kwa kutumia uwezo wetu binafsi kukabiliana na hali hii tukidhani uzoefu wetu utatusaidia kutatua matatizo hayo?kama ilivyokuwa kwa watu wale baharini pale pia ni dhahiri pamoja na uzoefu wetu hatutaweza kukabiliana na kutatua matatizo yetu bali hali itazidi kuwa mbaya zaidi.

Na,tunapokuja kukumbuka kuwa tumekabidhi maisha yetu kwa Yesu kristu na kwamba yu pamoja nasi muda na wakati wote,tunapopambana na majaribu,mateso,vikwazo,kukataliwa,kutengwa,kushindwa hata kukashifiwa na kudharauliwa kama jina lake "Mungu yu pamoja nasi" Yesu atatushuhudia tukishinda vikwazo na kuininuliwa,pamoja uhaba wa imani tulionao yeye ni mwingi wa rehema na fadhili zake ni za milele.