Monday, January 14, 2013

BWANA, TUOKOE, TUNAANGAMIA!!

Akiwa ufukweni mwa bahari ya Galilaya,kristu aliendelea kuhubiri injili na kutangaza ufalme wake,umati mkubwa ulikuwa mahali hapo ukitaka kuendelea kusikiliza ujumbe mzuri na wenye kufariji uliokuwa ukitoka katika kinywa cha Bwana, Yesu alikuwa akifafanua mafumbo aliyotumia kuuelezea ufalme wa mbinguni aliokuwa amekuja kuuanzisha,akitumia "habari ya mpazi",pia akiufananisha ufalme wa mbingu kama "mbegu ya aladali" na vilevile fumbo la "nyavu za kuvulia samaki".

Baada ya shughuli hii pevu ambayo bwana aliifanya kwa kipindi kirefu pasipo kula wala kunywa aliamua kuuondosha umati huo uliokuwa ukimsikiliza nakutafuta mahali ambapo angepata pumziko,Yesu aliwaamuru wanafunzi wake wapande mashua na kuelekea ng'ambo ya pili ya bahari katika mji wa Genesareti,mji ambao kristu aliendesha shughuli zake bila upinzani mkubwa hivyo aliamini angeweza kujipumzisha vizuri bila usumbufu wowote,katika kupanda mashua,idadi kubwa ya umati bado ilikuwa ufukweni pale na wakati wafuasi wa Yesu wakipanda mashua,watu waliokuwa wakitaka kuendelea kumsikiliza Kristu nao walipanda mashua yao kwani palikuwa na mashua zingine zilizokuwa zikitumika kwa shughuli ya uvuvi na punde safari ikaanza.

Kutokana na uchovu mkubwa pamoja na njaa,kwani kwa siku nzima Yesu alikuwa akihubiri injili pasipo kutia kitu chochote kinywani mwake,mara baada ya kupanda mashua jioni ile aliamua kutafuta mahali tulivu akajipumzisha na usingizi ukampitia.

Kitambo kidogo baada ya safari kuanza jua lilizama, ghafla giza nene likatanda mawinguni,ngurumo kali na radi zikaanza kupiga,upepo kutoka milimani na kimbunga cha ajabu kilianza,mawimbi yalianza kuzipiga mashua walizokuwa wakisafiria.....Miongoni mwa wafuasi wa yesu na umati uliokwa katika mashua zingine pia walikuwa ni watu waliokuwa wakifanya shughuli za uvuvi kwa karibu maisha yao yote,hivyo waliamini hali ile ni ya kawaida na kwamba baada ya muda mfupi bahari ingetulia kama mwanzo,lakini kadri muda ulivyokwenda hali ilizidi kuwa mbaya na mawimbi yalikuwa yakizipiga mashua nazo zikaanza kujaa maji.

Wafuasi pamoja na umati wa wtu katika mashua zile walijaribu kutumia uzoefu wao wa muda mrefu kukabiliana na hali ya hewa wakisahau ni nani aliyewaamuru kupanda katika mashua na kuelekea ng'ambo ya pili,baada ya kufanya jitihada zote na kushindwa maisha yao yalikuwa mashakani kwani mashua zilijaa maji na kuanza kuzama ghafla wakakumbuka kuwa ndani ya mashua alikuwamo aliyeshinda nguvu za mwovu,aliyekemea na kutoa mapepo hata kufufua wafu ndipo hapo wakaamua kumlilia wakiita kwa sauti..


Wafuasi/umati;  "Bwana,bwana...."Tunaangamia na wewe hutujali!!!!!"


Kwa kipindi hicho chote cha dhoruba baharini,Yesu alikuwa amelala usingizi,wafuasi wake walimtafuta lakini kutokana na giza na mahali alipokuwa amelala haikuwa rahisi kupatikana,mpaka mwanga mkali wa radi ulipo mulika ndipo walipomwona mwana wa Mungu amepumzika,ishara ya amani na upako wa Mungu vikidhirika katika usoni pake wakamwendea na kumwamsha wakimlilia kwa kutahamaki wakisema...

Wafuasi/umati;  "Bwana, tuokoe, tunaangamia!!!!!".


Kelele na vilio vya wafuasi na umati wa watu katika mashua zote zilimwamsha Bwana Yesu,kwani mawimbi yalizisogeza karibu mashua hizo hivyo kupelekea vilio na kelele za watu wenye hitaji la kuokolewa kusikika,mara Yesu akaamka na kusimama katikati ya wafuasi wake kisha akawaambia.

Yesu;  "Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba?"

Yesu alipoamka hakuwa na woga katika mwonekano wala maneno yake na wakati akizungumza maneno hayo,bado kelele na vilio viliendelea kusikika na kudhihirisha uhaba wa imani kwa watu wale,Mara Yesu akaondoka, akazikemea pepo na bahari kwa kunyoosha mkono wake wa kuume juu akasema.

Yesu;  "Amani,kuwe shwari"

Ghafla kukawa shwari kuu,mawingu yalisambaa,mwezi ukachomoza,nyota zikang'ara na giza likatoweka,upepo ukatulia,ngurumo zikanyamaza,radi, kimbunga vikakoma na mawimbi yakatulia bahari ikawa shwari,Wafuasi na umati wa watu wakamaka wakisema.

Wafuasi/umati;  "Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?"


Je, ni mara ngapi hali kama hii hututokea? kama ilivyokuwa pale baharini,giza linapotanda katika maisha yetu(sintofahamu),kimbunga cha maisha kinapoanza (majaribu),ngurumo na radi za maisha zinapotukabili (vitisho) na mawimbi yanapotuyumbisha (misukosuko) nasi kama watu wale hujaribu kwa kutumia uwezo wetu binafsi kukabiliana na hali hii tukidhani uzoefu wetu utatusaidia kutatua matatizo hayo?kama ilivyokuwa kwa watu wale baharini pale pia ni dhahiri pamoja na uzoefu wetu hatutaweza kukabiliana na kutatua matatizo yetu bali hali itazidi kuwa mbaya zaidi.

Na,tunapokuja kukumbuka kuwa tumekabidhi maisha yetu kwa Yesu kristu na kwamba yu pamoja nasi muda na wakati wote,tunapopambana na majaribu,mateso,vikwazo,kukataliwa,kutengwa,kushindwa hata kukashifiwa na kudharauliwa kama jina lake "Mungu yu pamoja nasi" Yesu atatushuhudia tukishinda vikwazo na kuininuliwa,pamoja uhaba wa imani tulionao yeye ni mwingi wa rehema na fadhili zake ni za milele.

Monday, December 24, 2012

ASILI YA YESU KRISTU

Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu.
Ibrahimu alimzaa Isaka; Isaka akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake; 

Yuda akamzaa Peresi na Zera kwa Tamari; Peresi akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu; 

  Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni akamzaa Salmoni;
Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese; 

Yese akamzaa mfalme Daudi.
Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa;
Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; 

Uzia akamzaa Yothamu; 
Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia; 

 Hezekia akamzaa Manase; Manase akamzaa Amoni; Amoni akamzaa Yosia;
  Yosia akamzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli.
 Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli;Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori; 

 Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi;
  Eliudi akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo;
  Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye Kristo.
 Basi vizazi vyote tangu Ibrahimu hata Daudi ni vizazi kumi na vinne; na tangu Daudi hata ule uhamisho wa Babeli ni vizazi kumi na vinne; na tangu ule uhamisho wa Babeli hata Kristo ni vizazi kumi na vinne. 

 Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 

  Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. 

 Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 

  Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. 

  Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema,Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe;  asimjue kamwe hata alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake YESU.

Tuesday, December 18, 2012

MAMBO HAYA YAWEZEKANA VIPI?

Akiwa kiongozi wa ngazi ya juu katika taifa la wayahudi,msomi na mwenye utajiri mkubwa lakini pia alikuwa mmoja kati ya wajumbe katika kamati za maamuzi katika nchi ya Israel,mtu huyu jina lake Nikodemasi...Kwa kipindi kirefu alikuwa amesikia habari kuhusu Mnazareti aliyekuwa akihubiri injili na wokovu kwa wana wa Israel huku akiweka wazi kuwa mamlaka yake si ya dunia hii na wala hakuja kuanzisha ufalme wa kupita katika hii dunia bali ufalme wake ni wa mbiguni....

Kwa macho yake alijionea namna ambavyo Yesu alisafisha hekaru la Bwana na kuwafukuza mafarisayo waliogeuza matumizi yake kutoka kuwa sehemu a kumwabudu Mungu na kulifanya kuwa sehemu ya kufanyia biashara na kuwadhulumu wanyonge....Akiwa mjumbe katika uongozi wa wayahudi,Nikodemasi aliwashauri viongozi wenzake kwamba isingekuwa busara kumpinga hata kutaka kumuangamiza Yesu wa Nazareti kwani maneno,matendo na nguvu zake zilidhihirisha alikuwa na utashi wa mungu na kwa kufanya hivyo wangejiweka katika laana kama ambavyo vizazi vilivyopita vilijiletea laana toka kwa Mungu kwa kuwapinga manabii aliowatuma lakini viongozi wenzake hawakumwelewa....

 Baadae,aliamua kufanya mazungumzo na Yesu ili apate uelewa zaidi juu ya mamlaka aliyokuwa anataka kuianzisha hivyo kwa kuhofia kuonekana na watu kuwa kiongozi wa wayahudi akipata maelekezo toka Kwa Yesu na pia kuepuka kuwashawishi watu wengine kufanya kama kiongozi wao tena wa ngazi ya juu aliamua kuomba mazungumzo ya falagha na Yesu na alifanya hivyo kwa kumtafuta wakati wa usiku katika milima ya sayuni mahala ambapo Bwana alipatumia kwa mapumziko,alipofika mazungumzo yao yalikuwa kama ifuatavyo..


Nikodemasi; "Rabbi, Najua kuwa wewe ni Mwalimu na ni mtu mwenye upako wa hali ya juu kwa maana hakuna mtu awezaye kutenda mambo uyatendayo isipokuwa nguvu za Mungu ziwe pamoja naye"

Aliamua kutumia maneno ya sifa ili kujipa ujasiri pia kumfanya Yesu atambue kuwa alikuwa anamheshimu na kutambua uwezo wake,kumbe pasipo kujua alikuwa anafanya kosa ambalo hata katika kizazi hiki linatendeka,kosa la kumtambua kristu kama mwalimu atokae kwa Mungu wakati Yesu kristu ni Mungu mwenyewe alikuja kwa njia ya kimwili ili awakomboe watu wake ndiyo maana jina lake "Emmanuel" yaani Mungu pamoja nasi...Lakini Yesu tayari alikwisha tambua mawazo ya Nikodemasi na ndani yake aliona mtu mwenye kiu ya kutaka kujua ukweli,naye alimtazama machoni akamwambia...

Yesu; "Hakika nakwambia,Isipokuwa mtu azaliwe kutoka Mbinguni,hatauona ufalme wa Mungu"

Kwa maneno haya,Bwana Yesu alikuwa akimaanisha kwamba,Binadamu hawezi kwenda mbinguni kwa kutimiza sheria tu na mtu yeyote ambaye anjitahidi kuishi maisha yake kadri sheria inavyomwelekeza kwa lengo la kuuona ufalme wa Mungu anajaribu kufanya jambo lisilowezekana....Nikodemasi alizidi kuchanganyikiwa  na akauliza swali..

Nikodemasi; "Mtu awezaje kuzaliwa tena angali mkubwa?"

Yesu; "Hakika nakwambia,Isipokuwa mtu azaliwe upya kwa maji na roho, Ataangamia"

Nikodemasi aliskia mahubiri ya Yohana mbatizaji juu ya ubatizo kiroho akisema "mimi nawabatizeni kwa maji, lakini yupo ajae yeye atawabatiza kwa moto ambaye sistahili hata kutembe katika nyayo zake" akakumbuka kuwa katika taifa la Israel watu waliokuwa wamepokea ubatizo waliwachukulia kama watu waliokuwa wamezaliwa na hivyo walihitaji kukua zaidi kiroho hivyo alijua wazi kuwa Yohana alikuwa akimzungumzia Yesu kristu wa nazareti....Wakati akitafakari,Yesu alimtazama Nikodemasi na kugundua kuwa,ukweli ulikuwa ukipata makazi ndani yake na akaamua kutumia upepo kumwelewesha juu ya kuzaliwa upya...

Yesu; "Upepo huvuma kutoka sehemu moja kuelekea sehemu nyingine,lakini mtu hawezi kuelezea upepo huo unavuma kutoka mahali fulani kwenda mahali fulani bali mtu anaweza kutambua matokeo ya upepo huo kwani huyumbisha matawi na kudondosha majani ya miti,vivyo hivyo mtu hawezi kuelezea muda wala namna ambavyo amezaliwa kiroho"

Ufalme wa mbingu hatutaurithi kwa kurekebisha makosa yetu na kujaribu kutii amri za mungu katika roho ile ile bali ni lazima tupokee roho mpya wa mungu ambaye atabadilisha mfumo mzima wa maisha yetu na hazina zetu tutazielekeza mbinguni na kutafuta vitu vya kudumu visivyoonekana kwani vitu vyote tuwezavyo kuvigusa na kuviona kwa macho si vya kudumu bali vinapita tu...Kufikia hapa.Nikodemasi alikuwa kimya pamoja na mazingira yalivyo katika milima ya sayuni milio ya ndege na ubaridi ulitawala usiku ule,kutaka kufahamu zaidi akauliza tena..

Nikodemasi; "Mambo haya yawezekana vipi?"


Swali kama hili na mengine mengi yanayohoji mambo ya kiroho,halikuulizwa na yeye tu,bali hata katika jamii yetu hivi sasa tunapoishi,kuna watu wamepata kusikia habari hii ya kuzaliwa upya kiroho lakini wameruhusu mbinu za mwovu ambae huwafanya wasiwe na imani na wamekuwa wakiuliza kama Nikodemasi "mambo haya yote yawezekana vipi?"...majibu yao ni sawasawa na jibu ambalo Yesu alimpatia Nikodemasi...

Yesu; "Wewe ni kiongozi,msomi na mwenye mali lakini hujui kama mambo haya yawezekana...mambo haya yawezekana na hii kwa wenye imani kwani mwanadamu wa kawaida hawezi akatambua mabo ya kiroho,mambo ya kiroho hutambuliwa kiroho na ni kama upuuzi kwake na kamwe hawezi kuyatambua,kwani ndani yake hutoka hisia za tamaa, chuki na wivu kama ndani yake hutoka hisia kama hizi ni nani awezae kuzalisha kitu kizuri kutokana na kitu kibaya,hakuna hata mmoja! na hujui ya kwamba kupenda ya dunia ni kumchukia Mungu."

Kanuni hii ya kuzaliwa kiroho ni muhimu sana kwa mtu kuwa mjinga hata asiielewe,hivyo Yesu alishangaa kuona Kiongozi wa Wayahudi hajui kama mambo haya yawezekana kwani wayahudi walikuwa wanaamii kuwa wao ni uzao wa Ibrahim Baba wa mataifa,hivyo walidhani wanastahili kuurithi ufalme wa mbingu na njia waliyoamini ilikuwa ni kutii sheria,kitu ambacho Yesu kristu alipokuja walimpinga kwani alihubiri injili ya wokovu kwa mtu yeyote atakae amini....Nikodemasi alionesha kutoelewa na hapa Yesu akamwachia ujumbe muhimu na kuthibitisha kuwa yeye hakuja kuvunja agano bali kukamilisha yaliyotabiriwa na kuashiriwa...

Yesu; "Kama nimekwambia mambo ya Dunia hii hujanielewa,itakuwaje endapo nitakwambia mambo ya mbinguni? sikuja kuanzisha ufalme duniani bali  ufalme wangu ni wa mbinguni"...

Nikodemasi alimshukuru Kristu kwa kukata kiu yake na kumpa ufahamu mkubwa,aliamini kuwa Yesu wa Nazareti ndiye masia aliyetabiriwa katika maandiko na aliendelea kufunua maandiko ili kujua zaidi na akazidi kuamini hata wayahudi walipopanga kifo cha Kristu alikuwa akiwakumbusha kufunua maandiko ili watambue kuwa walikuwa wakitaka kufanya maamuzi ambayo wangeyajutia lakini shetani alifunga akili,macho hata masikio yao hatimaye wakatimiza yaliyoandikwa "mwana wa Mungu atasalitiwa mikononi mwa wanadam"...Baada ya kristu kusulubiwa,Nikodemasi alikumbuka maneno ya Yesu aliyomwambia usiku ule "mwana wa Adamu atainuliwa juu" akajua utabiri na maandiko yametimia akaamua kumhabarisha Mtakatifu Mathayo naye akaandika habari hii na ikawekwa katika Biblia Takatifu Agano Jipya.


Kama ambavyo Mussa alinyanyua nyoka wa shaba jangwani ili wana wa Israel waweze kumtazama na nyoka waliokuwa wakiwaangamiza wasipate kuwadhuru,vivyo hivyo mwana wa Adamu atainuliwa juu...kama Mussa alivyoinua juu nyoka wa shaba mfano wa nyoka waliokuwa wakiwaangamiza wana wa Israel,pia mwana wa Adamu kwa mfano wa mwenye dhambi ambazo zinatuangamiza wanadamu leo atainuliwa juu...kama ilivyokuwa jangwani,ili kutokuangamizwa na nyoka Mungu alimwambia Mussa "waambie wana wa Israel wamtazame nyoka wa sahaba na hawataangamia" Mungu pia anatuambia mimi na wewe leo tumtazame mwana wa Adamu aliyeinuliwa Msalabani kwa ajili ya dhambi zetu na sisi hatutaangamia...Hakuna maelezo mengi wala uthibitisho wa kisayansi juu ya maagizo ya Mungu kupitia kwa nabii wake pale jangwani ni kutazama na kupona au kutotazama na kuangamia....hapa pia hakuna maelezo wala ufafanuzi wa kitaalamu ni kuamini na kuishi au kutoamini na kuangamia.

Saturday, December 1, 2012

HATUTAKUFA,TUTALALA TU!

Miongoni mwa wafuasi vipenzi wa Yesu,alikuwa mtu mmoja aitwae Lazaro,mwenyeji wa Bethani....Lazaro alikuwa anampenda na kumwamini kristu kwani kazi na miujiza aliyokuwa akiitenda ni kielelezo tosha kilichomfanya aamini kuwa neno limekuwa hai na maandiko yalikuwa yanatimia kama jina lake "mungu pamoja nasi" lilivyo basi kristu na maisha yake yote aliyoishi ilikuwa mungu ameamua kujidhihirisha kwa wanadamu ili waweze kumwamini na wapate kukombolewa kutoka katika dhambi iliyokuwa imewafunga na kuwatesa watu wake.


Lazaro alikuwa na dada zake wawili Maria na Martha,hawa pia walimpenda na kumwamini mwokozi vilevile kristu alikuwa anawapenda sana wanandugu hawa na familia yao yote ka ujumla,mara nyingi alipokuwa amechoshwa na kundi kubwa la watu waliokuwa wakimfuata na shida zao hata pale ambapo alizongwa na waliokuwa wanampinga kwa nia ya kumuangamiza kristu alitafuta pumziko katika familia ya wapendwa hawa,hivyo kulikuwa na upendo wa dhati kati yao kama mwokozi na wafuasi wake.

Ghafla siku moja Lazaro alipatwa na ugonjwa mkali hata akawa mahututi kitandani,dada zake,ndugu jamaa na marafiki walikuwa wakijitahidi kufanya kila liwezekanalo ili kuokoa maisha ya mpendwa wao,walijaribu kila tiba na dawa lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya.Ilitokea kama maajabu kwamba ndugu hawa wajaribu kumtibu ndugu yao wao wenyewe wakisahau kwamba kwa macho yao walipata kumwona mwana wa mungu akiponya kila aina ya magonjwa.


Baada ya kujaribu kila walichoamini kingeweza kuokoa maisha ya ndugu yao bila mafanikio yoyote,kumbukumbu ilimjia Maria dada yake na Lazaro kwamba kimbilio pekee la suluhisho la kaka yao ni Yesu....Faraja kubwa iliwajaa mioyono mwao baada ya Maria kutoa wazo kwamba upelekwe ujumbe kwa Yesu juu ya hali ya Lazaro,wote walijua jinsi Yesu alivyompenda Lazaro hivyo waliamini mara apatapo ujumbe huo angefika mara moja na kumponya.


Akiwa anaendelea na kazi yake ya kuhubiri injili ya wokovu katika miji mingine kristu pamoja na wanafunzi wake,mara akawajia mtu mmoja akiwa na ujumbe usemao "Bwana,tazama yule umpendae yu mahututi kitandani"...Yesu alipokea ujumbe ule kisha akamuamuru mjumbe aliyeleta habari zile arudi bila kumpa jibu lolote,alipofika Bethani,Maria,Martha watu wote walikuwa wakimngoja kwa shauku wakidhani Yesu angesitisha shughuli zake na kwenda kuwafairiji lakini hawakuamini macho yao walipomwona kwa mbali aliyekuwa amepeleka habari kwa yesu juu ya hali ya rafiki yake kipenzi Lazaro akirejea mnyonge akiwa peke yake bila majibu wala taarifa yoyote,walihuzunika sana lakini ndani ya mioyo yao faraja ya mungu iliwajaa hata hawakumlaumu yesu kwa kutowajali....Baada ya mtu aliyeleta ujumbe kuondoka zake,kristu akawaambia wanafunzi wake


Yesu;  "Twendeni katika mji wa Yudea,huko nako tukahubiri injili"


wanafunzi wake walimjua Lazaro na jinsi alivyompenda na kumwamini Yesu hivyo walishamgazwa sana na namna ambavyo yesu alizipokea habari za ugonjwa wake,wakahoji....


Wanafiunzi; "Bwana, tazama yule umpendae yu mahututi kitandani lakini wataka twende Yudea, je umesahau jinsi ambavyo wanakutafuta ili wakuangamize katika mji wa Yudea"?


 Yesu; "Siku ina masaa 24,hivyo basi muda wangu pia haujawadia,hamjui ya kwamba mtu hutembea mchana kwani mwanga humwongoza,lakini yule atembeaye katika giza nuru ya mbingu humwongoza?"


Wanafunzi wake walimheshimu Yesu na kuamua kuongozana naye hadi katika mji wa Yuda,huko walikaa kwa takribani siku tatu....Wakati huohuo kule Bethani hali ya lazaro ilizidi kuwa mbaya na hatimaye akafariki.... Dada zake walilia kwa uchungu kwani walimpenda sana kaka yao,mafarisayo na wale waliokuwa wakimpinga Yesu waliwakebehi na kuwacheka chinichini dada wa Lazaro kwa kile ambacho walidai Yesu aliwaterekeza lakini mioyoni mwa Martha na Maria kulikuwa na faraja ya kipekee na waliamua kumwachia na kumtukuza mungu kwani yeye alimpenda zaidi kaka yao.....Baada yataarifa za kifo cha Lazaro kumfikia,Yesu akihubiri injili ghafla akawaita wafuasi wake,akawaambia


Yesu; "jiandaeni twende katika mji wa Bethani nyumbani kwa Lazaro"


Wanafunzi; "Bwana, kuna haja gani ya kwenda ili hali Lazaro amekwisha kufa?"


Yesu; "Ni bora mmejua kuwa amekufa, hii imetokea ili kwa macho yenu mjionee na muweze kuamini"


Safari ilianza kuelekea Bethani,si umbali mrefu sana kutoka walipokuwa na walipokaribia nyumbani kwa Lazaro, Maria aliona kundi la watu likijongea katika msiba huo uliokuwa umejaa watu wengi kwani Lazaro alikuwa mtu maarufu na familia yao ilikuwa na ndugu na jamaa wengi.....tayari maandalizi ya mazishi yalikuwa yamefanyika na mwili wa Lazaro ulikuwa umeoshwa vizuri,umepakwa mafuta na kuvishwa sanda tayari kwa kuzikwa....Maria alipoona kundi lile alijua wazi ni Yesu na wanafunzi wake pamoja na waliomfuata huku na kule,maria alimkimbilia Yesu,alipomfikia akamwangukia miguuni akilia,akasema...


Maria; "Bwana, kama ungekuwapo Lazaro asingekufa"


Yesu; "Usilie, Lazaro hajafa bali amelala tu"


Yesu alipomwambia Maria "Lazaro amelala tu" watu wengi wakiwemo waliokuwa wakimwamini na ambao walikuwa hawamwamini na kumpinga Yesu na kwa masikio yao wenyewe walimsikia yesu akimfariji Maria kwa kumwambia kuwa kaka yao hajafa bali alikuwa amelala tu,Maria alikwenda kumwambia Martha kwamba mwokozi alikuwa amefika kuwafariji na mara baada ya kupata taarifa hizo Martha alifurahi na huzuni yote ilitoweka...Watu wote waliofika msibani pale walitambua kuwa binadamu mwenye nguvu na upendeleo wa mungu alijumuika nao,kwani tangu kristu afike mahala pale utulivu ulitawala,vilio na huzuni viligeuka kuwa nyimbo na mapambio,malaika wa mbinguni walikuwa wametanda katika anga lile na mwili wa Lazaro ulikuwa ndio chombo muhimu ambacho kwa mara nyingine tena Yesu anathibitisha kuwa hakika yeye ni mwana wa mungu....waliomwamini Yesu walikuwa na furaha sana mioyoni mwao kwani walijua wazi nguvu za mbingu zitathibitika tena mahala pale,lakini waliompinga walihofia na kuogopa kwani kadri yesu alivyotenda miujiza watu walimwaini na kumsifu mungu.........Tazama,yesu akasema...


Yesu; "Mmeuweka wapi mwili wa Lazaro?"


Maria; "Ndani ya nyumba hii"


Yesu; "Basi watu wote wakae nje na wachache tuongozane hadi ulipo mwili"


Hapo Yesu,Maria,Martha na watu wazazi wao wakamwongoza kristu hadi mahali ambapo waliulaza mwili wa Lazaro,wakakuta umezungushiwa sanda maalum kwani muda mchache baadae walikuwa wakijiandaa kwenda kuuzika,yesu akasogea karibu na mwili wa Lazaro, akainua kichwa chake juu,akafungua mikono na viganja vyake akamwomba baba yake wa mbinguni kwa dakika chache, kisha kwa sauti kali iliyochoma masikio ya watu wote mahala pale na kupenya katika masikio ya Lazaro aliyekuwa amekufa,akaita..


Yesu; "Lazaro amka!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!"


Taratibu,Lazaro aliyekufa siku tatu kabla,ambaye damu ilisimama kutembea mwilini mwake,ambaye macho yalifumba,masikio yaliziba na pua zake hazikupumua  alifumbua macho,masikio yalifunguka,pumzi yake ilirejea na damu ikaanza kutembea mwilini mwake kama mwanzo,akaininuka na yesu akamshika mkono akamwinua na akawaambia watu waliokuwa pale..


Yesu; "mfungueni sanda, mumpatie mavazi yake na chakula ale"


Wakamfungua sanda na kumvisha mavazi safi,Lazaro alionekana mwenye furaha na amani ya mungu ndani yake na Yesu alimkabidhi kwa dada zake Maria na Martha  pamoja na wazazi wao.....vilio,huzuni,upweke na nguvu za mwovu vilikuwa historia mahala pale kwani nderemo,vifijo na ufalme wa mungu ulitawala na watu wote walimuamini Yesu na kumtukuza mungu...


Mpendwa,kama hujapokea zawadi ya mungu ya wokovu hujachelewa fanya hivyo sasa kwa kumpokea na kumwamini Yesu kristu kama mfalme na mwokozi wako na mara baada ya kumwamini Yesu,roho mtakatifu atakujia ndani yako ambaye ataishi milele ndani yako na kukuthibitishia ufufuko,wokovu na kukushirikisha katka makazi ya milele huko mbinguni,maandiko yanasema "siku ya mwisho kristu atapaza tarumbeta mawinguni na watu wote wataisikia sauti yake,walio wafu watafufuliwa na kwa wale waliomwamini atawachukua na kwenda nao mbinguni kwa mungu baba,lakini kwa wale wasioamini watakwenda kuzimu...

Tuesday, November 13, 2012

NIKUTENDEE JAMBO GANI?

Akipita katika lango kuu la Yeriko kuelekea Yerusalem mahali ambapo alijua wazi kwamba atasalitiwa na kumwaga damu mikononi mwa wanadamu,Yesu akiwa ameongozana na wafuasi wake pamoja na watu wengi walioufuata msafara wake,hii ilikuwa safari yake ya mwisho kabisa kupita katika lango hilo na kwa takribani miaka mitatu alikuwa amekamilisha kazi ya kueneza injili na hivyo wakati ulikuwa umewadia wa mwokozi wetu kuinuliwa na kutukuzwa.

Yeriko ni lango la barabara inayoingia katika mji mkuu wa Yerusalem,hii ni barabara maarufu na kama hali ilivyo katika barabara zetu hii leo, watu wasiojiweza na wenye ulemavu hukaa pembezoni mwa barabara kuomba misaada kwa wapita njia ndiyo hali ilivyokuwa katika barabara ya Yeriko. Miongoni mwa wasiojiweza na walemavu hao alikuwapo kipofu ambaye kwa ulemavu wake huo, mkono wa mungu ulidhihirika na kuufanya umati ulioshuhudia muujiza huo kumtukuza mungu.

Upofu ulikuwa ugonjwa ulioambatana na ukoma na jamii ya wayahudi waliamini kuwa mtu mwenye ukoma ni mtu ambaye pengine kutokana na dhambi zake mwenyewe au wazazi wake alikuwa na laana ya mungu,hivyo vipofu na wakoma walitengwa,walinyanyaswa na kunyimwa haki zao za msingi.Miongoni mwao alikuwepo kipofu aliyekuwa amesikia habari zilizoenea kwa kasi kwamba Yesu kristu anatenda miujiza na kuponya magonjwa sugu pia kuwafungua waliofungwa na vifungo vya mwovu, kipofu huyu anajulikana kwa jina la Bathoromayo.

Kama inavyoaminika kwamba vipofu wana uwezo mkubwa sana wa usikivu na utambuzi wa sauti,mara baada ya kusikia kelele na vishindo vya umati wa watu walioambatana na Yesu, Bathoromayo alijua wazi kuwa wakati wa muujiza wake umewadia na akaanza kuita akisema.....

Bathromayo: "Yesu!,yesu!,yesu!,yesu!!!!!!!......"


Kutaka kutambua mtazamo wa umati ule juu ya watu wa tabaka la chini, Yesu pamoja na kumuona na kumsikia kipofu Bathromayo alimpita hata akaufanya umati ule udhani kuwa alikuwa mwenye haraka sana nao watu walithibitisha kuwa hawakutambua kazi na wajibu wa mwana wa mungu, wakamdhihaki na kumkatisha tamaa Bathromayo wakimwambia..

Umati: "Kimya wewe uliye laaniwa,hutambui kwamba yu mwenye haraka?"


Kwa kuwa hawakuwatambua na kuwathamini walemavu ,baada ya kusikika akiita jina la yesu Bathromayo alinyamazishwa na kumriwa akae kimya mara moja,lakini hakukata tamaa akaendelea kulia kwa sauti kubwa.....

Bathromayo: "Yesu!!!!!! mwana wa Daudi,nionee huruma!!!!"

 
Kuudhihirishia umati ule kwamba,mungu amemuinua kristu kuhubiri injili kwa wanyonge,waliotengwa na jamii,kuwaweka huru waliofungwa na vifungo vya mwovu na kutangaza wokovu kwa mataifa yote, mara akasimama na kumwita.....Bathromayo alitupa shuka lake pekee aliliokuwa akijisitiria kwa kipindi hicho chote cha upofu kwani alijua kuwa wakati wa muujiza wake ulikwisha wadia na kamwe hatalihitaji tena shuka lile.....alipofika,Yesu akamuuliza...


Yesu: "Nikutendee jambo gani.....?"

Bathromayo: "Nipate kuona !!!!!!!!!!!!!"

Yesu alimuuliza Bathromayo swali hili ili kupima imani aliyokuwa nayo juu yake ,jibu lake "nipate kuona tena" ni kielelezo kuwa imani aliyokuwa nayo juu ya kristu ilizidi hata imani ya wale waliokuwa wakimfuata na kushuhudia miujiza yote aliyokuwa akitenda kwani Bathromayo hakupata nafasi ya kujionea kwa macho bali kwa kusikia tu aliamini....Baada ya kusikia jibu lile na kutambua imani kubwa aliyokuwa nayo,Yesu kwa mikono yake miwili alimgusa macho yake na kumponya akisema.....
 

Yesu; Imani yako imekuponya,umesamehewa dhambi zako zote


Mara baada ya mguso na neno moja tu la kristu,macho yaliyokuwa yamefumba kwa takribani miaka thelathini yalifumbuka,akapata kuiona tena taswira ya dunia na kumwona aliyemtendea miujiza sura yake yenye upako iking'ara kwa miale ya mbinguni,akanyanyua macho yake yaliyoponywa na kutazama juu mbinguni akaona mwezi na kumtukuza mungu kwa machozi na furaha akisema.

Bathromayo: "Nimeonaa!!!!! nimeona!!!!"


Yesu; Usimwambie mtu yeyote juu ya mambo haya, bali utimize mapenzi yake mungu baba aliye mbinguni."

Umati: "Haaa,ni maajabu!!!!!,hata vipofu wanaponywa,hakika huyu ndiye masiya!!!!! miujiza!!!!!"

Yesu: "kwa nini hamuamini, lipi jambo gumu kwenu, au hamuamini ya kwamba mwana wa mungu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi.....? Hakika nawaambieni yeyote mwenye imani aweza amuru mti huu ung'oke na ukatuame baharini na ikawa kama alivyonena, bali tu mkiomba ombeni kwa jina langu naye baba wa mbinguni atajibu maombi yenu kwani mimi ndiye njia, kweli na uzima  na hakuna awezae kufika kwa baba pasipo kupitia kwangu."

Kisha Yesu, wafuasi wake pamoja na umati wa watu waliokuwa wakimfuata wakaendelea na safari yao kuelekea katika mji wa Yerusalem naye Bathromayo akaungana nao na kuwafuata huku akimsifu yesu na kumshukuru mungu kwa mambo aliyomtendea...


Ndugu yangu,mpendwa mkristu mwenzangu yawezekana wewe si kipofu lakini kama Bathromayo unalo tatizo, pengine unasumbuliwa na ugonjwa, umetengwa na jamii, umesalitiwa na uwapendao, umekataliwa, umasikini unakutatiza, ni mjane, ni yatima, umeathirika na madawa ya kulevya na pombe au umefungwa na vifungo vya mwovu, TAMBUA kwamba usomapo habari hii ni wito wako na Yesu anakuuliza "akutendee jambo gani?" Yawezekana kuna watu, vitu, hali au mazingira fulani yanakufanya ukate tamaa na usiweze kupata baraka zako toka kwa bwana kama ambavyo umati wa watu ulivyomkatisha tamaa Bathromayo, nakusihi jipe noyo THIBITISHA imani yako kwa kumkabidhi yeye mzigo uliokuelemea, naye kwa mguso au neno moja atakwenda KUKUPONYA, KUKUFARIJI, KUKUWEKA HURU, KUKUSAMEHE DHAMBI ZAKO ZOTE na  KUKUPA UZIMA WA MILELE.

Thursday, November 1, 2012

JIRANI YANGU NI NANI HASA?

Katika kile kinachoaminika kuwa ni kutafuta chanzo  ili wapate sababu na misingi ya kuweza kujitetea kwa kumkana mwana wa mungu,Wayahudi walikuwa wakimuuliza maswali ya mtego bwana wetu Yesu kristu, pasipo kujua kwamba Yesu alikuwa anatambua mawazo yao kabla hata hawajazungumza chochote, pia  kwa kudhani kuwa walikuwa wakimuuliza maswali ya mitego, kumbe walikuwa wakidhihirisha kuwa hawakua na uelewa juu ya mambo ya kiroho, bali shetani alikuwa akiwatumia kukwamisha mpango wa mungu, kupotosha jamii na kugeuza dini ya mungu kuwa njia ya kutimiza matakwa na maslahi yao binafsi



Hivyo katika kile walichoamini wao ni kutaka kumtega ili waweze kupata sababu za kumhukumu yesu kristu,siku moja akiwa anafundisha neno la mungu,wanafunzi, wafuasi pamoja na kundi kubwa la watu kutoka sehemu mbali mbali waliokuja kwa nia ya kufunguliwa na kupata suluhisho juu ya matatizo yao, alijijitokeza mwanasheria mmoja miongoni mwa mafarisayo waliokuwa wakimpinga mwana wa mungu na kumuuliza swali, mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo.



Mwanasheria; Je,nitafanya nini ili nipate kuuona ufalme wa mungu?


Yesu;  Mpende bwana mungu wako,kwa moyo wako wote,kwa akili zako  zote na kwa uwezo wako wote, utapata kuuona ufalme wa mungu

Mwanasheria; Nimekuwa nikifanya hivyo maisha yangu yote, nitende kipi cha ziada?
       
 
Yesu; Basi mpende jirani yako,kama unavyojipenda.


Mwanasheria; Jirani yangu ni nani hasa?



Hapa ndipo mwana wa mungu alipotumia mfano wa kweli na hakika ili kuweka wazi juu ya utata wa nani hasa ni jirani kwa enzi zile hata katika maisha yetu hivi leo, akaanza kwa kusema.



"Mtu mmoja mwenyeji wa Yerusalem alikuwa akisafiri kwenda katika mji wa Judea,alipofika katika lango kuu maeneo ya Yeriko,watekaji nyara walimvamia,wakampora kila alichokuwa nacho na kumjeruhi vibaya kisha wakaondoka zao na kumwacha mahututi. Muda mfupi baadae akapita mtumishi wa mungu, alipomwona majeruhi yule alimtazama akapita pembeni na kwenda zake akielekea hekaruni,baada ya muda si mrefu tena akapita mzee wa kanisa naye akamtazama mtu yule aliyekuwa mahututi  na kupita pembeni kisha akaenda zake pia akiwahi katika nyumba ya ibaada....Baada ya kitambo kirefu kidogo,mtu mmoja mwenyeji wa Samaria akiwa safirini kuelekea nchi ya mbali kupitia Yerusalem alipofika katika eneo la tukio na kumkuta majeruhi yule yu mahututi hajitambui,aliteremka katika farasi wake akambeba majeruhi yule na kwenda nae katika sehemu ya kupumzikia wageni akamkanda majeraha yake kwa maji ya moto na kumpaka mafuta, akampatia tiba madhubuti hata akapata fahamu na kujitambua,  kisha akamlipa mwenye nyumba ile ya kupumzikia wageni na kumwambia "mhudumie mgonjwa huyu na nirejeapo toka safarini nitalipia gharama zote ,kisha akaenda zake,aliporejea kutoka safarini alilipa gharama zote".



Kutoka katika habari hii,iliyopo katika Biblia takatifu katika kitabu cha mtakatifu Mathayo,utaona kwamba kulikuwa na hali ya uadui mkubwa sana kati ya Israel na Samaria kwa ajili ya Wayahudi kuamini kuwa wao ni taifa teule la mungu na mtu yeyote asiye na asili ya Israel hasa wa Samaria alionekana hana thamani machoni mwao na mungu wao pia......Lakini wao wenyewe wameshindwa kutambua thamani na umuhimu wa ndugu na Myahudi mwenzao aliyekua amevamiwa na kujeruhiwa vibaya na kumpita kwa haraka ya kufika katika nyumba za ibaada na kusahau kutoa msaada kwa kiumbe wa mungu ambaye wanamsujudu.....pengine walitawaliwa na hofu ya kuvamiwa pale au kuhusishwa na tukio hilo,tofauti na Msamaria aliyeamua kutoa msaada kwa majeruhi yule bila kujali itikadi,utaifa, wala hofu ya kutekwa na kuhusihwa na tukio hilo......


Baada ya kumaliza kusimulia habari hiyo ambayo ndiyo chanzo halisi cha neno maarufu ambalo hadi leo hii tunalitumia "msamaria mwema",Yesu akamuuliza mwanasheria yule.


Yesu; Je,kati ya hawa watatu nani ni jirani ya mtu huyu aliyekuwa mahututi....?


Mwanasheria; Yule Msamaria...


Yesu; Basi na wewe tenda kama Msamaria huyu na utapata kuuona ufalme wa mungu..

Nasi katika maisha tunayoishi leo,ni muhimu kutambua kwamba,si kwa nafasi,wadhifa au vyeo katika dini au jamii tunayoishi na wala si kwa kumpenda mungu wetu, kwa mioyo yetu yote, kwa akili zetu zote na uwezo wetu wote tu, bali kwa kumpenda jirani yetu pia, kama Msamaria mwema alivyofanya, tukikumbuka kuwa hatuwezi kumpenda mungu tusiyemuona pasipo kumpenda binadamu mwenzetu tunayemuona.

Saturday, October 6, 2012

ZUNGUMZA NA MUNGU

Mungu ni mwema,tena ni mwaminifu,ana upendo mkubwa sana kwetu,huruma na rehema zake hazina mfano, fadhili zake ni za milele na uweza wake hauelezeki kwani kwake hakuna lisilowezekana,ametuumba kwa mfano wake na alipotuumba akatupa utaratibu wa kuufuata katika maisha yetu hapa duniani ili ajitukuze na baadae atushirikishe katika maisha ya milele huko mbinguni.

Katika historia ya mwanadamu,mwenyezi Mungu amekuwa akiwasiliana nasi kwa njia mbalimbali kama vile matendo,ishara au viashiria tofauti na hali ilivyokuwa kwa Adam binadam wa kwanza ambaye kabla hajamkufuru Mungu alikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja yaani aliweza kuiona sura ya Mungu na kusikia sauti yake.baada ya Adam kumkufuru Mungu hakuweza kuiona tena sura wala kuisikia sauti badala yake Mungu alitumia manabii,mitume na watakatifu kuwasiliana na wanadamu.


NENO LA MUNGU
Biblia ni neno kutoka kwa Mungu kuja kwetu wanadamu kupitia manabii,mitume na watakatifu ambao Mungu aliwajaza upako ili waweze kuelezea asili, hisia, mtazamo, mpango wa Mungu juu yetu wanadamu pamoja na ujio wa mwanae yesu kristu,neno la Mungu ni kweli hakika mbingu na nchi vitapita lakini neno litasimama daima.Katika neno lake Mungu ametupa maagizo namna ya kuishi na kumpendeza yeye aliyetuumba.


Mpendwa mkristu mwenzangu,ni vizuri kukumbuka kuwa tunaweza kuzungumza na Mungu kwa namna mbili tofauti na kuzungumza bila imani, katika uzungumzaji wa namna hii watu tunasoma neno, tunafanya maombi, sikiliza mahubiri na kuyaacha hapo hapo bila kujifunza chochote,hali ni tofauti na kuzungumza kwa imani ambapo tunatakiwa kusikiliza  na kusoma neno, kufanya maombi, kulitafakari, kuamini na kulifanya neno kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku.Wakati wote tukizungumza na Mungu kwa imani ni muhimu kutenda haya yafuatayo.

KUTAFAKARI
Wakati tunazungumza na  Mungu iwe ni kwa kusoma au kusikiliza neno lake ni muhimu sana kutafakari juu ya maana ya maandiko husika na nini yanamaanisha ikiwa ni pamoja na kugundua namna ambavyo tutafanya maandiko hayo kuwa sehemu ya maisha yetu.

KUOMBA
Biblia haisomwi kama vitabu vingine vyote,ni muhimu kabla ya kuisoma tumwombe Mungu atuwezeshe kusoma na kuelewa pia atuongoze katika maandiko yanayohusu hali tunayopitia katika kipindi husika katika maisha yetu ili kupitia neno lake azungumze nasi na kutusaidia kupata ufumbuzi wa suala husika.

KUNYENYEKEA
Tunapokuwa tunazungumza na Mungu iwe kwa kusoma,kusikiliza hata kwa sala na maombi ni muhimu kuwa wanyenyekevu, maana yake ni kuwa tunapoomba hatuombi kikaidi na tunapomwomba tukitegemea atatujibu maombi yetu kama mapenzi yake yalivyo.

KUTUMAINI
Ahadi za mungu tunazozisoma katika neno lake au kusikiliza kupitia kwa watumishi wake hakika ni za kweli na wakati ukitimia mungu atatenda, hivyo tuwapo katika maombi tunatumaini kuwa kwa wakati wake mungu baba atajibu maombi yetu.

KUWA NA SUBIRA
Katika historia ya mwanadamu,maandiko yanaonyesha namna mungu alivyokuwa anatenda miujiza na kujibu maombi kwa watu wake, lakini majibu ya maombi hayo hayakuja kama mvua ni kipindi kirefu kinahitajika pengine mungu huwa na maeneo ambayo anayafanyia marekebisho au kutaka kurekebisha wasifu wetu ili baraka zake zitufae zaidi,hivyo subira ni sifa muhimu sana kwetu sisi kama wakristu.

ZUNGUMZA NA MUNGU LEO
Mpendwa,umeshatambua kuwa Mungu anahitaji kuzungumza na wewe leo juu ya maisha yako hapa duniani na mbinguni pia? kama hujatambua, chukua uamuzi sahihi sasa kwa KUSOMA neno lake lililo katika biblia takatifu, pia ili uweze kukua kiroho ni muhimu kwa KUSIKILIZA mahubiri, hivyo tafuta kanisa jirani yako ambalo yesu kristu ndiyo mwokozi na mfalme na ujiunge, kwa kujumuika na wakristu wenzako utazidi KUAMINI na kupitia imani yako ndiyo utazidi kuuona mkono wa Mungu ukitenda miujiza katika maisha yako na wewe utazidi KULITENDA neno..

Monday, October 1, 2012

UDHAIFU WA SHETANI

Mwenyezi mungu baada ya kumaliza kazi nzito ya kuiumba dunia pamoja na vitu vyote vilivyomo ndani yake,kazi iliyokuwa imebaki ni kutuchukua na kutushirikisha katika maisha ya milele huko mbinguni,kwa kushirikiana na mwanae mpendwa yesu kristu mfalme wa amani ambaye ndiye aliye na mamlaka yote duniani na mbinguni pia,chini yake alikuwa huyu ambaye sisi leo hii tunamtambua kama shetani mfalme wa nguvu za giza.


Upendo wa mungu kwetu sisi wanadamu ni wa ajabu na hauna mfano na mambo aliyotuandalia huko mbinguni hayajawahi ingia akilini wala hayajawahi onekana kwa macho wala masikio yetu hayajawahi kusikia,maandiko yanasema itakuwa furaha na shangwe......Shetani kwa tamaa ya madaraka kwani alitaka kuwa juu ya mwana wa mungu pamoja na wivu kuona kuwa mungu anatupenda sana sisi wanadamu kuliko hata malaika,akaamua kumsaliti muumba na kufanya hivyo aliapa ya kwamba kamwe mimi na wewe tusiuone upendo,baraka,huruma,rehema za mungu pamoja na ufalme wa mbingu.Mungu baba akaamua kumuadhibu kwa kumtupa duniani, kisasi cha mungu kipo juu yake na siku ya mwisho atakwena jehanamu.

HANA MAMLAKA
Maandiko yanasema mbingu na dunia na vyote vilivyo ndani yake vinavyoonekana na visivyoonekana ikiwa ni pamoja na shetani mwenyewe vimeumbwa na mungu na yeye ndiye mwenye mamlaka yote,hakuna kiumbe yeyote aliye juu ya mamlaka aliyoianzisha mungu wa majeshi na kumkabidhi mwanae yesu kristu.

HANA NGUVU
Baada ya kutupwa duniani na mungu,shetani alinyang'anywa nguvu zote na kwamba hana uwezo wa kuukwamisha mpango wa mungu kwetu sisi wanadamu wa kwenda mbinguni,kabla ya ujio wa yesu kristu shetani aliwatesa sana na kuwabebesha mizigo ya dhambi wanadamu kwa nguvu za giza,lakini mara baada ya ujio wa mwana wa mungu,shetani na nguvu zake za giza hana uwezo wa kututesa tena kwani jina la yesu ndiyo jina lenye nguvu kushinda majina yote.

NI MUONGO
Hapa duniani dhambi imeletwa na shetani ambaye ni mfalme wa nguvu za giza kwani utakumbuka kuwa baada ya mungu kumpatia Adamu msaidizi wake Eva aliwapa sharti moja muhimu ya kwamba wale matunda yote katika bustani aliyowakabidhi isipokuwa tunda la mti wa katikati,shetani(mfalme wa uongo)akamdanganya Eva kuwa endapo watakula tunda kutoka katika mti wa katikati watakuwa na nguvu sawa na mungu hivyo kwa uongo wa shetani,Adam na Eva wakatenda dhambi.

ANA WIVU
Biblia inasema kuwa upendo,huruma na rehema za mungu kwetu ni za ajabu,pamoja na kwamba sisi hatutambui upendo na huruma aliyonayo mungu juu yetu haimaanishi kuwa atatuacha, ndiyo maana alimtoa mwanae wa pekee ili atukomboe,ni upendo wa ajabu kwani sisi ndiyo wakosaji lakini bado mungu ametupa msamaha bure kwa wote watakao amini jina la yesu.Shetani anajua ukweli huu na ana wivu juu ya upendo huu wa muumba kwetu ndiyo maana halali anakesha kutugombanisha na mungu.

NI MSALITI
Katika mpango huu mwema wa mungu,shetani huyuhuyu alikuwa ni mshirika,tena mmoja kati ya washirika wa juu lakini kwa tamaa ya madaraka na wivu,akamsaliti mwenyezi mungu,hata anapowatumia wanadamu hujidhihirisha kama mtu mwenye kusahau fadhila na kuwasaliti watu wake wa muhimu,unajua kila kitu kuhusu Yuda kwani pamoja na kuwa mwanafunzi wa yesu kwa takribani miaka mitatu wakitembea huku na kule akiona miujiza yote aliyokuwa akitenda kristu na kuthibitisha kuwa yeye ndiye massiah,lakini shetani alimshawishi hadi akamsaliti mwana wa mungu kwa vipande thelathini vya sarafu.

NI MUOGA
Katika safari zake yesu akiwa na wanafunzi wake popote walipokwenda,kwa kujua uwezo wake watu wenye matatizo mbalimbali walimfuata aweze kuwafungua na kuwaponya toka katika kifungo cha huyu mfalme wa uongo aliyewatupia mapepo na magonjwa sugu wafungwa hawa wa shetani mara walipokuwa wakihisi uwepo wa mtakatifu mwana wa mungu na mfalme wa amani,pepo hao walilia kwa uoga na kuhamaki hata kumuomba bwana awaruhusu wawaingie wanyama na kutoweka mara moja.

ANA CHUKI
Katika kizazi chote cha mwanadamu kilio,mateso,maumivu na vikwazo vimekuwa ndiyo njia na mbinu ya mwovu huyu kutufanya tusifurahie na kutambua upendo na huruma ya muumba wetu,ni kwa sababu shetani ana chuki dhidi yetu sisi wanadamu,hututupia mapepo,hutufanya tuwe na tamaa,wasiwasi na hofu juu ya dhambi zetu kitu ambacho mungu kwa huruma na rehema zake ametupa msamaha na kuzitupilia mbali dhambi zetu.

ANATUMIA NGUVU ZA GIZA
Shetani hututisha kwamba anaweza kutudhuru au kutukwamishia baraka na neema zetu zitokazo kwa mungu,lakini nakuhakikishia mkristu mwenzangu shetani hana nguvu zozote bali ni muongo na matendo yake yote ni matendo ya nguvu za giza na kwamba nguvu zetu sisi ni kubwa kuliko zake kwani mara atakapotukabili tu,tunampambanisha na mfalme wa nguvu za mwangani yesu kristu ambaye jina lake lapita majina yote.

ATATUPWA JEHANAMU
Maandiko matakatifu yanasema kwa wale ambao hawatamtii mungu na kuheshimu amri zake kwa kupenda mambo ya kupita katika hii dunia kwa kumfuata shetani,wao pamoja na kiongozi wao wote watatupwa jehanamu katika moto wa milelele sehemu ambayo maandiko yanasema itakuwa ni kulia na kusaga meno.


NGUVU ZA YESU KRISTU
Wapo wanadamu waliodanganyika kwa kuamua kumfuata shetani na nguvu zake za giza wakidhani kuwa atawatatulia matatizo yao pasipo kujua kuwa wanajiweka katika hatari ya kisasi cha mungu kuwa juu yao,nakushauri mwanadamu mwenzangu chukua uamuzi sahihi sasa kwa kumwamini na kumfuata yesu kristu kwani ana MAMLAKA duniani na mbinguni pia,ana NGUVU kushinda shetani kwani amekabidhiwa na mungu mwenyezi, ni KWELI kwani yesu kristu ni neno la mungu lililo hai,ahadi yake ya kuja kutuchukua ni ya kweli na ataitimiza kwani ni MWAMINIFU,alipoagizwa na mungu kuja kutukomboa sisi wanadamu alimkabili shetani na kuishinda dhambi pale kalvari kwani ni JASIRI,popote alipokwenda alikuwa akiwafungua na kuwaponya watu waliokuwa wamefungwa na kuteswa na shetani kwani kristu ana UPENDO wa kweli juu yetu,miujiza yake yote anayotenda ni mungu hutenda kwa NGUVU ZA MUNGU kwani hivi sasa YUKO MBINGUNI  ameketi kuume kwa mungu baba na atakuja kutuchukua mimi na wewe.

Tuesday, September 25, 2012

HERI YAO

Katika jamii yetu ni kawaida sana kusikia mtu akisema "heri yao" huku akiendelea kwa kutaja baadhi ya mambo au vitu ambavyo pengine ni muhimu sana katika maisha tunayoishi lakini katika ufalme wa mbingu si chochote......kwa mfano,ni kawaida kusikia mtu akisema heri ya wale wenye pesa nyingi,heri ya wale wenye elimu,heri ya wale wenye ajira au heri ya wale wenye afya njema na mambo mengine kadha wa kadha.......katika maisha yake mwokozi wetu yesu kristu aliishi maisha bila dhambi na maisha yake tangu kuzaliwa, kusulubiwa, kufufuka hadi kupaa kwake mbinguni, kristu alionyesha namna mungu alivyo na upendo,huruma hata nguvu na uweza uliotukuka ndiyo sababu aliitwa "Emmanuel" likiwa na maana "Mungu pamoja nasi"

Matendo yake,mwenendo wake, uweza wake  hata maneno yake kristu ni kielelezo juu ya matendo,mwenendo na uwezo wa mungu. Basi ni dhahiri kwamba maneno aliyoyatamka mwokozi wetu yesu kristu hakika ni maneno toka kwa mungu mwenyezi na moja katika ya maneno muhimu aliyoyatamka ni yale ambayo aliyotamka wakati akiwafundisha wanafunzi wake pale kilimani akisema.

HERI YAO MASIKINI WA ROHO
Katika mstari huu,kristu alimaanisha wale wenye kutambua umasikini wao katika mambo ya kiroho,mambo yahusuyo mwenyezi mungu na ufalme wa mbingu kwa ujumla,watu hawa wapo tayari kusikiliza,kusoma,kutafakari,kuamini na kulitenda neno la mungu.Watu hawa waliotambua umasikini wao wa kiroho ndiyo ambao mungu huwapa uwezo wa kutambua mambo hayo kwani "mwanadamu wa kawaida hatambui mambo ya kiroho,ni kama upuuzi kwake na kamwe hawezi kuyaelewa kwani hutambuliwa kiroho.

HERI YAO WENYE HUZUNI
Huzuni yaweza kusababishwa na matatizo,magonjwa,mateso pia majaribu ya hii dunia,katika neno lake mungu baba ameweka wazi kuwa chanzo cha yote hayo ni dhambi, hivyo huzuni husababishwa na dhambi ndiyo maana kristu alisema heri wenye huzuni lakini hii ni kwa wale waliotambua chanzo cha huzuni hiyo kuwa ni dhambi na kuamua kutubu na kupokea wokovu kwa kumwamini na kumfuata yesu.

HERI YAO WAKARIMU
kweli, wacheshi na wapole twaweza kuwaweka katika kundi la wakarimu,lakini katika mafunzo yake pale kilimani kwa wanafunzi wake yesu kristu alisema hata ukawa na imani ya kuweza kuhamisha milima, kama huna upendo ni sawa na bure,ukarimu huu alioumaanisha bwana ni hali ya kuwa na upendo kwa wanadamu wenzetu,alisema mpende jirani yako kama unavyojipenda pia akasisitiza mpende adui yako.

HERI YAO WENYE NJAA NA KIU YA UTAKATIFU
Biblia inasema "hakuna mwanadamu awezae kuishi maisha bila dhambi bali mmoja tu aliye mtakatifu"naye ni bwana wetu yesu kristu,lakini bwana alisema kuwa, heri ya wale ambao mioyo yao ina njaa na kiu kubwa ya kuishi maisha takatifu,maisha ya kumpendeza mungu,maisha katika kristu,biblia inaendelea kusema kuwa "watakatifu watapimwa kwa imani"hivyo twaweza potoka katika dhambi lakini imani yetu i ndani ya kristu na kwamba amezilipa dhambi zetu zote pale msalabani hivyo kwa kuteswa kwake si tumekuwa watakatifu.

HERI YAO WENYE HURUMA
Tunapoishi maisha katika dunia hii,shida na mateso ni vitu visivyoepukika,maandiko yanasema "katika dunia hii mtapata mateso,lakini vumilieni kwani nimeushinda ulimwengu" ni neno la mungu kuhusu uwepo wa mateso katika maisha yetu,hivyo kristu anasema wale ambao huguswa na mateso ya wengine kama vile wajane,yatima,wagonjwa,waliofungwa,masikini na wote wanaoteseka na shida za hii dunia kwa kuwatembelea,kuwafariji na kuwapatia misaada baraka zao zipo.

HERI YAO WENYE MOYO SAFI
Twaweza kuwa wapole,wacheshi,wakarimu hata wenye upendo lakini tusiwe na mioyo safi....moyo safi hutokana na kupokea zawadi ya wokovu kutoka kwa mungu,zawadi hii ni kumpokea na kumwamini yesu kristu kama mwokozi na mfalme katika maisha yetu,mara baada ya kamwamini yesu kristu mioyo yetu humpokea roho mtakatifu ambaye hutufundisha na kutuwezesha kutenda mema na kuepuka dhambi na hapo ndiyo mioyo yetu inaweza kumpendeza mungu.

HERI YAO WENYE AMANI
Amani moja kati ya matunda ya roho mtakatifu,akiwa ndani yetu hutuwezesha kuwa na imani ndani ya mioyo yetu pamoja na shida,njaa,chuki,wivu,tamaa,vita,magonjwa na tabu tunazokabiliana nazo katika  hii dunia..kristu alipowaambia wanafunzi wake "heri wenye amani" alikuwa anamaanisha amani ya kiroho na si kutokuwepo kwa shida au matatizo ya hii dunia na amani hii ni zao la roho mtakatifu pekee,hivyo kwa wale tuliompokea kristu amani i tele ndani ya mioyo yetu.

HERI YA WALE WANAOHUKUMIWA KWA AJILI YA UTAKATIFU
Tunapoishi maisha katika kristu ni lazima tupambane na upinzani mkubwa kwani biblia inasema "dunia hupenda ya dunia,hivyo mkiona mnachukiwa mjue kuwa nyinyi si wa dunia kwani mngekuwa wa dunia, dunia ingejipenda" ndiyo maana wayahudi hawakuweza kuutambu awakati ambao mwokozi alikuja kupitia jamii yao na wakashindwa kutii maandiko juu ya aliyetabiriwa (kristu) hata wakati mtakatifu Yohana akimbatiza yesu na sauti toka mbinguni ikasikika ikisema "huyu ndiye mwanangu mpendwa,msikilizeni" hawakuamini, matokeo yake wakamhukumu mwana wa mungu na israel ikashindwa kupokea heshima kuwa kitovu cha dunia kwa kushindwa kutambua wakati wa ujio wa kristu.



Katika ufalme wa mbingu kila tendo lina matunda yake liwe jema ua baya,hivyo tunapoishi maisha katika kristu tusichoke kutenda mema kwani baraka na neema za mungu zatufuata popote tuendapo,ni muhimu kukumbuka kuwa twaweza pata matunda mengi mema kwa kutenda mema hapa duniani lakini malipo haswa yatungoja mbinguni pale ambapo mwokozi wetu yesu kristu atakuja tena kutuchukua sisi tulio hai na wale walio wafu watafufuliwa kwenda mbinguni kwa mungu baba.



Japokuwa kristu alipendelea kuwafunza wanafunzi wake kwa mafumbo,lakini hapa aliweka wazi juu ya mambo ambayo mungu atatenda kwa watu wake,hii ni katika kuonyesha umuhimu na msisitizo wa jambo lenyewe, napo akasema.......Heri ya masikini wa roho maana UFALME WA MUNGU NI WAO......Heri yao wenye huzuni maana WATAFARIJIWA........Heri yao wakarimu maana WATARITHI UFALME WA MBINGU.......Heri wenye kiu na njaa ya utakatifu maana WATASHIBISHWA.........Heri wenye huruma maana WATASAMEHEWA........Heri wenye mioyo safi maana WATAMWONA MUNGU.......Heri wenye amani maana WATAITWA WANA WA MUNGU..Heri wanaotengwa na kuhukumiwa kwa ajili ya utakatifu kwa maana UFALME WA MBINGU NI WAO.

Thursday, September 6, 2012

AHADI YA MUNGU KWAKO


 Upendo wa mungu kwako

mpendwa mkristu mwenzangu......hebu jiulize swali,kitu gani kinafanya Mungu atende au adhihirishe mkono wake katika maisha ya wanadamu.....?je ni wema au uzuri wetu.....?La hasha,mkono wa Mungu unadhirika katika maisha yetu kwa sababu moja tu ya misingi kuwa yeye aliupenda ulimwengu hata akaamua kumtoa mwanawe wa pekee na yeyote atakae mwamini ataishi milele......hata hivyo Mungu ni mwema na fadhili zake ni za milele ahadi yake katika maisha yetu ni kutulinda,kutubariki,kutuokoa,kutuinua,kutuwezesha na kutusamehe dhambi tutendazo hivyo ni lazima tuwe na imani kamilifu juu ya uaminifu wa Mungu kuwa atatimiza ahadi yake kwetu, lakini pia ni muhimu kujiuliza ni kitu gani kinachompelekea Mungu kutenda kwa kuhusisha namna ambavyo alijitokeza katika maisha ya manabii na maisha yetu leo.

Mpango wa mungu kwako

Mungu alituumba kwa makusudi yake ili kumpa utukufu yeye aliye juu,hivyo katika kila jambo tulitendalo sisi tuliempokea Yesu kristu kama mwokozi na mfalme wa maisha yetu ni kwa ajili ya utukufu wake na kwamba yu pamoja nasi akitulinda,kutubariki na kutuwezesha ili tutimize mpango huo na kumpa utukufu yeye aliyetuumba....katika  ahadi zake juu ya kutimiza mpango wake na kujiinua katika maisha yetu Mungu hakutuhakikishia kutokuwepo na upinzani wala vikwazo kwani shetani ameapa kutupotosha sisi wanadamu ili Mungu asipate utukufu lakini pasipo kujua Mungu hutumia vikwazo,matatizo na upinzani wa shetani kutupatia ushindi watu wake na vilevile kujitukuza yeye mwenyewe.

Ahadi ya mungu kwako

 
Wokovu, baada ya adam na eva kumkufuru Mungu,kizazi chote kiliandamwa na laana ya dhambi iliyopelekea kutengwa na Mungu,lakini yeye alitoa ahadi ya kutukomboa na ulipowadia wakati kwa uwezo wa roho mtakatifu alizaliwa Emmanuel " Mungu pamoja nasi" mfalme wa amani ambaye wayahudi walimkana na kumsulubu pasipokujua walikuwa wakitimiza mpango wa wokovu kwetu sisi wanadamu kwani kwa kupigwa kwake sisi tumeokolewa.

Msamaha, hata baada ya mpango wa wokovu kutimia kwa bwana Yesu kulipia dhambi zetu zote mslabani,bado wanadamu laana ya dhambi inatuandama na kamwe hatutaiepuka bila damu ya Yesu, habari njema ni kwamba msamaha upo kwa wale watakaotubu dhambi zao na kumwamini Yesu kristu.

Uponyaji,  maisha ya bwana wetu Yesu kristu ni kielezo juu ya Mungu na namna upendo wake juu yetu ulivyo mkubwa...mahali pote Yesu alipotembelea aliponya vipofu, viziwi, walemavu, wakoma,hata kutoa mapepo kwa kuwagusa tu watu waliokuwa wakisumbuliwa na magonjwa au matatizo mbalimbali, kwa kufanya hivi alikuwa  akitimiza ahadi ya Mungu ya uponyaji kwa watakao amini.

Baraka, Mungu ameahidi kuwabariki watu wake lakini hii ni kwa wale wanaomwamini na kumtegemea Yesu kristu kwani kwa kumwamini yeye utajiwa na roho mtakatifu atakaye kupa ufahamu juu ya utendaji na miujiza ya Mungu na kukuwezesha kutenda na kuishi maisha yanayompendeza Mungu.

ulinzi, Mungu yupo kila mahali na kila wakati yu pamoja nasi,anajua mwanzo hata mwisho juu ya kila kitu kinachohusu maisha yako na yangu pia, habari njema ni kwamba anatupenda na kutujali na zaidi ya yote ameahidi kutulinda dhidi ya maadui wanaotukabili sasa hata baadae na atageuza kila ambacho kwa hali ya kawaida inaonekana kama hatari na kuwa ushindi kwetu na utukufu kwake.

Uwezeshaji, nguvu za Mungu hudhihirika baada ya kikomo cha uwezo wa mwanadamu, katika kila jambo ambalo linaendana na mpango wake juu ya maisha yetu mungu ameahidi kutupatia nguvu ya kuamua na kutenda pia, bila kujali vikwazo wala mazingira magumu, Mungu atatuwezesha kutimiza yale aliyotupangia kwa utukufu wake.

Kutuinua, kuwa wakristu hakutuepushii matatizo, vikwazo, chuki na mateso ya hii dunia lakini kwetu sisi tulio na imani tunajua ya kwamba Mungu atatuinua kwa kugeuza aibu, huzuni na fedheha zetu kuwa furaha na shangwe mara baada ya utukufu wa bwana wetu Yesu kristu kudhihirika.

Mungu anatimiza ahadi yake kwako leo
Mpendwa nakuomba uanze kwa kumpokea na kumwamini Yesu kristu kuwa mwokozi wako na mara baada ya kutubu dhambi zako ahadi ya WOKOVU itakuwa imetimia kwani ni bure na haki ya kila anayekiri kuwa Yesu ni mwana wa Mungu............usihofu juu ya dhambi utakazotenda kwani MSAMAHA upo kwa wale wanaoamini kwani hakuna hukumu juu ya wale walio katika kristu,wale watendao kiroho na si kimwili.........magonjwa yanayokusumbua,mapepo uliyorushiwa,laana uliyorithi,vifungo ulivyofungwa vyote vinakwenda kutenguliwa kwani kristu ANAPONYA tatizo linalokusumbua.........Kwa chochote unachofanya iwe ni Elimu, Biashara, Kilimo na hata Ajira unakwenda kufanikiwa kwani BARAKA za mwenyezi Mungu zinakufuata popote uendapo mradi tu unachokifanya kimtukuze na kiwe katika mapenzi yake.........Asubuhi, mchana na jioni wewe , watoto wako, ndugu jamaa na mali zako zipo chini ya ULINZI maalum kwani damu ya Yesu inayo nguvu zaidi ya adui yeyote anayekusudia kuwadhuru..........usitazame elimu yako, ujuzi wako, uwezo wako wala mazingira yanayokuzunguka kwani Mungu ATAKUWEZESHA kutimiza kile alichoahidi katika maisha yako.......ni kweli umasikini unakutesa, watu wamekucheka, umehuzunika na kufedheheshwa vya kutosha nakuambia kuwa Mungu anakwenda KUKUINUA leo.

Thursday, August 23, 2012

KABLA MUNGU HAJAKUBARIKI


 NANI AMEBARIKIWA?

 Mtu mwenye mwonekano mzuri au sura nzuri,mali nyingi,cheo au afya njema ndiyo mtu aliyebarikiwa na Mungu?.....Ukweli ni kwamba kila mmoja wetu katika kristo amebarikiwa kwani baraka ni uwezo wa kiroho ambao tunaupata kutoka kwa Mungu ili kutuwezesha kusonga mbele katika maisha ya imani pamoja na shida, vikwazo, vishawishi, majaribu na mateso tunayokabiliana nayo. Katika kitabu cha mtakatifu Mathayo Yesu kristo anasema wamebarikiwa maskini wa roho, wenye moyo safi, wenye imani, wenye huzuni na wanaoteswa na kuonewa kwa ajili ya utakatifu.Ukweli ni kwamba hakuna binadamu yeyote anayeweza kuishi katika dunia hii bila kutegemea neema za mwenyezi Mungu, Hivyo mimi na wewe tunahitaji sana neema na baraka za Mungu.

KABLA MUNGU HAJAKUBARIKI. 

Ni kweli kwamba ili tuvune mazao yatubidi tupande mbegu,ili mvua inyeshe mawingu sharti yatande,ili kiumbe kizaliwe mbegu mbili ya kike na kiume ziungane, hali hii ni asili katika maisha yetu.Ukweli ni kwamba kabla Mungu hajatubariki katika maisha yetu pia hutenda mambo ya msingi yafuatayo:

Hupima imani
Imani yako ni kithibitisho cha mambo yasiyo onekana, kigezo juu ya mambo yajayo na tusipokua na imani hatuwezi kumpendeza Mungu.Ukweli ni kwamba imani yetu ndiyo kipimo cha baraka zetu tutakazopokea, kumbuka Ibrahim kabla Mungu hajambariki kuwa baba wa mataifa yote alipima imani yake katika kiwango cha hali ya juu kabisa kwani ulipita muda mrefu sana kabla ahadi ya Mungu haijatimia, pia alimpima kwa kumwamuru amtoe sadaka mwanae wa pekee Isaka.

Huruhusu majaribu
Majaribu ni wakati ambao tunakua tunapambana na wakati mgumu pengine kiroho hata kimwili, kiasili majaribu tunaweza kuyaleta sisi wenyewe au Mungu huruhusu yatokee katika maisha yetu, majaribu hupima upendo na  imani yetu kwa Mungu.Kumbuka Ayubu alijaribiwa katika kiwango cha juu kabisa kwani Mungu alimruhusu shetani aangamize watoto, mifugo na mali zake zote, kama haitoshi aliruhusu magonjwa kwa Ayubu.

Huruhusu mateso
kipigo,njaa,kiu, kumwaga damu, kifungo na usaliti,ilimradi tu roho itambue utukufu wa Mungu na kumlilia kumbuka katika bustani ya getsemane walimkamata, wakampeleka kwa Pilato, kwa Herode baadae kwa pilato tena akabeba msalaba hadi golighota, akasulubiwa na saa la tatu tetemeko la ardhi, radi na giza nene vilithibitisha 'imekwisha' akakata roho.... Huyu ni Yesu kristo mwana wa Mungu.

Hutoa wajibu
Wajibu ni kazi au majukumu ambayo yatupasa kuyatimiza katika maisha yetu kama wafuasi wa kristo ,imeandikwa asiyefanya kazi na asile,kumbuka Nuhu Mungu alimpa wajibu wa kujenga safina hatua mia tatu urefu, upana sabini na awaingize viumbe wawili wawili na mimea wa kila aina ndani ya safina, Mungu alimwagiza kujenga safina akasema ataamuru mvua kubwa na mafuriko  katika taifa ambalo mvua haikuwahi kunyesha karne kadha zilizopita.

Huleta maadui
Adui anaweza kuwa binadamu, mnyama au kitu chochote ambacho hutokea mbele yako kikihatarisha uwepo wako, maendeleo yako au hata afya yako.Kumbuka Daudi alikua mchunga kondoo, chini ya miaka kumi na nane aliyeagizwa kupeleka chakula cha wapiganaji waliokuwa wakijianda lakini kwa hofu kumkabili aliyekuwa kiburi katika vita mfilisti Goliathi.Daudi kwa imani alikusanya mawe kadhaa na kombeo lake na akamkabili Goliathi.

Huleta upinzani
Iwe kiroho au kimwili mtu au kitu kinachotenda kinyume na wewe au shughuli au kazi yako, sote huelewa na kupenda upinzani katika michezo kwani huburudisha,lakini upinzani aliopambana nao Saulo ambaye baadae aliitwa Paulo hakika ni wa ajabu dharau kuchekwa,kupigwa mawe, kulala nje,kunyeshewa na mvua, njaa, kufungwa jela,mijeledi na upinzani hatari dhidi ya kueneza injili ya yesu.

Husubiri utayari
Uwezo, imani na utayari wako katika kupokea baraka na neema za Mungu ni muhimu sana kabla hujapokea baraka hizo kumbuka mungu ni mwaminifu na kamwe hawezi akaruhusu baraka zitakazotuathiri hivyo ni lazima tuonyeshe utayari wa kuzipokea, kumbuka kipofu aliyekaa katika milango ya Yeriko akiwa ombaomba tangu kuzaliwa kwake aliposikia kelele za msafara wa Yesu aliyekuwa amesikia habari juu ya yesu mponyaji na mwokozi alilia kwa sauti na kuita 'Yesu Yesu,mwana wa Daudi nionee huruma' mtu mmoja akajibu 'wacha utamchelewesha' kwani ile ilikua safari yake  ya mwisho kuelekea yerusalem, mara Yesu akasimama na kumwita, aliruka na kumfuata kisha Yesu akamuuliza 'unataka nikufanyie nini?'naye akajibu 'nipate kuona' ...jina lake ni Bathlomeo

JIANDAE KUBARIKIWA LEO. 

Mungu anakubariki leo, utapata nguvu na uwezo wa kushinda na kufanikiwa katika maisha yako.Mungu anajaribu IMANI yako kama Ibrahim alivyovumilia na kusubiri ahadi kwa muda mrefu, vumilia pia.....Mungu anaruhusu MAJARIBU katika maisha yako, kama Ayubu alivyovumilia baadae Mungu alimpa mara mbili ya alichopoteza,Vumilia pia utapata mara mbili zaidi ya ulichopoteza,...........Mungu ameruhusu MATESO kama yesu kristo aliteswa  akasulubiwa, akafa na siku ya tatu akafufuka yupo mbiguni na atarudi kutuchukua mimi na wewe..... Mungu amekupa WAJIBU,kazi kama ya Nuhu,alifanya kama Mungu alivyoagiza bila kujali watu walio mkejeli kwa kujenga safina katika nchi ambayo mvua haikunyesha kwa miaka mingi kabla, lakini alijenga na Mungu alileta mvua na ikawaangamiza wote isipokua Nuhu na familia yake, Timiza wajibu wako ambao Mungu amekupa na utabarikiwa,............Mungu ameruhusu MADUI kama Daudi aliamini Mungu angempa ujasiri wa kumkabili Goliathi ambaye alikua anamzidi nguvu, urefu, umri hata siraha hivyo basi usiangalie ukubwa wala hatari kuhusiana na maadui,watu,wanyama hali au vitu vyovyote.. mtegemee Mungu na si uwezo wako, kama Daudi utashinda maadui.
Mungu ameruhusu UPINZANI katika maisha yako, elimu yako, biashara yako, afya yako hata katika kazi yako,.........Paulo aliamua kuendelea kueneza injili ya Yesu ndiyo sababu sehemu kubwa ya agano jipya aliandika yeye vitabu kama warumi, wagalatia, wahebrania, wafilipi na waefeso na vingine vingi ambavyo leo vinasababisha mimi na wewe tunabarikiwa, hivyo usijali upinzani songa mbele
Mungu anangojea UTAYARI wako wa kupokea na kulinda baraka zake kwako, kama Bathlomeo aliposikia msafara wa yesu alithibitisha utayari na imani yake... zaidi ya kuona,  Yesu pia alimsamehe dhambi zake zote, nawe pia onyesha utayari wa kupokea baraka na neema za Mungu kwa kumlilia katika sala na maombi zaidi ya kubarikiwa utasamehewa dhambi zako zote.  

Friday, August 10, 2012

MAADUI na MWOKOZI


 Kumwamini yesu kristu kama mfalme na mwokozi wetu hakutaweza kutatua matatizo yetu yote,japo tutapata nguvu ya kiroho itakayotusaidia kupambana na matatizo hayo tuwapo hapa duniani,sote twatambua kuwa hatuwezi tukaishi katika dunia hii bila dhambi kwani ni Kristu pekee aliyeishi maisha bila dhambi pengine tujiulize ni kwa nini wanadamu tunatenda dhambi ili hali tunaelewa wazi kuwa Mungu anachukia dhambi.....?Jibu ni kwamba kuna maadui watatu ambao husababisha tumkosee muumba wetu,nao ni hawa wafuatao.
          
         SHETANI....Baadaa ya kutupwa duniani,shetani aliapa kutukosanisha sisi wanadamu na Mungu hivyo hutumia kila mbinu kutushawishi ili tutende dhambi,mbinu yake kuu ni uongo na hufanya kila njia ili kufanya mwanadamu asitambue baraka alizonazo kutoka kwa Mungu,shetani hututia huzuni,wasiwasi,woga,hofu ili tusiutazame utukufu wa Mungu,pia hutujaza tamaa,wivu,chuki,hasira ili tumkosee Mungu na wanadamu wenzetu.

          DUNIA.....Maisha tunayoishi katika dunia hii iliyomuasi Mungu hayatoweza kumpendeza Mungu....Binadamu na tabia zetu,utaratibu wa mambo ya kidunia na vishawishi vyake hutufanya tuishi ya dhambi na kumchukiza Mwenyezi Mungu.Maandiko yanasema "kupenda ya dunia ni uadui na Mungu"...mambo mengi yanayochukuliwa kama mambo ya  kisasa hupelekea kila mmoja wetu kunaswa katika dhambi mfano,mavazi yasiyofaa,filamu chafu,tamaa iliyokithiri ya pesa na madaraka,uchawi na nguvu za giza vyote hivi na vingine vingi hutuweka katika gereza la dhambi.

         MIILI YETU.......Mungu alituumba kwa mfano wa sura yake ili ajitukuze kupitia maisha yetu yakumpendeza tutakayoishi katika hii dunia kabla hajatuchukua na kutushirikisha katika maisha ya milele huko mbinguni,alitupa viungo mbali mbali na akaweka utaratibu wa namna ya kuvitumia kwani alijua wazi bila utaratibu huo tutapotoka...bahati mbaya miili hii ambayo ni hekaru la Roho mtakatifu tunaitumia vibaya kwa dhambi,mfano ulevi wa pombe,uzinzi,mauaji na anasa za dunia,maanndiko yanasema "hakika roho i tayari bali mwili hau tayari" ni kweli miili yetu inapingana na mapenzi ya mungu japo roho zetu zinampenda au la!

         maandiko yanasema "mshahara wa dhambi ni mauti" ni kweli kwamba kwa wenye dhambi wataishia jehanamu na walio okoka watakwenda mbinguni......"Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanae wa pekee ili atukomboe sisi wanadamu"ni kweli kwamba kutaka kuwa watakatifu katika dunia hii,na shetani akitupotosha huku miili yetu wenyewe inapenda anasa za dunia isingewezekana hivyo Mungu akamtuma mwane wa pekee aje atukomboe.

       YESU KRISTU........Wokovu ni bure na yeyote atakaye mpokea na kumwamini yesu kristu kama mwokozi na mfalme wake na kwamba alipokwenda msalabani alilipa dhambi zake,hakika ataishi milele...